Basata yawatoza faini Rayvanny, Diamond

Muktasari:

Basata imeufungia wimbo wa Mwanza pamoja na kuwatoza faina ya Sh9 milioni wanamuzikii Rayvanny, Diamond pamoja na lebo ya Wasafi

Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limewatoza faini ya Sh9milioni wanamuziki Rayvanny, Diamond na lebo ya Wasafi kutokana na maudhui ya wimbo wa Mwanza uliopigwa marufuku jana.

Hatua hiyo imekuja baada ya kufanyika kwa kikao kati ya wanamuziki hao na bodi ya Basata, kilichoketi kwa takribani saa tatu katika ofisi za baraza hilo zilizopo Ilala Jijini Dar es Salaam.

Katibu wa baraza hilo, Godfrey Mngereza amesema kiasi hicho cha fedha kimetozwa kwa wasanii wenyewe Rayvany na Diamond kila mmoja kutakiwa kulipa Sh3 milioni na lebo ya Wasafi ambayo nayo imesajiliwa katika baraza hilo.

Sambamba na hilo, Mngereza amesema wametakiwa kupeleka mashairi ya wimbo huo kwao na kusisitiza kuwa hakuna mahala utakaporuhusiwa kupigwa hapa nchini iwe usiku au mchana kwa kuwa haifai kusikiliza katika jamii.

"Huu wimbo haufai kabisa hata kwenye kikao tumemuuliza Rayvanny je unaweza kuimba mbele ya wazazi wako kajibu hapana, inaonyesha namna gani hata yeye anaona hauna maadili, tupige marufuku isipigwe halafu turuhusu ifanywe hivyo usiku?" Alihoji Mngereza.

Meneja wa lebo ya Wasafi, Hamis Taletale 'Babu Tale' amesema katika kikao walichokaa leo na Basata, yameamuliwa mambo mawili ikiwemo kupeleka mashairi ya wimbo huo yakahaririwe na kutoendelea kuusambaza wimbo.

Babu Tale amesema barua ya kuitwa kikaoni waliipata jana jioni na kati ya mambo waliokubaliana ni kupeleka mashairi ya wimbo huo.

Kuhusu kuufuta kwenye mitandao amesema hilo wataenda kulijibu kwa barua kama ambavyo wepewa barua na Basata.

Suala la wasanii wao kujitetea kupitia instagram, amesema wameona mambo yatakayozungumzwa kikaoni huenda yakabaki humo, hivyo wameamua kutumia platform ya mitandao kueleza utetezi wao.