Baraza: Simba itafika mbali kimataifa

Muktasari:

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza amekiona kikosi cha Simba kinaweza kikafanya vyema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiishauri wachezaji wao waongeze bidii zaidi.

KOCHA wa Biashara United, Francis Baraza amesema wachezaji wa Simba, wakiendelea na kiwango walichokionyesha dhidi yao, basi kimataifa anaona watafika mbali.

Simba iliishushia kichapo cha mabao 4-0 Biashara United kwenye Uwanja wa Mkapa, jambo ambalo kocha huyo, ameona linawafanya wachezaji wa Wanamsimbazi kujiamini na itawajenga kuelekea kimataifa.

Amesema haina maana kwamba kikosi chake kilikuwa hakipambanii pointi tatu, lakini anaona Simba ilicheza kwa kuelewana na wachezaji wake walijiamini zaidi.

"Simba inaelekea kimataifa ni kitendo chakuongeza umakini na wachezaji wake kuwa wazalendo zaidi kwa timu yao, naamini itafanya vyema kwani nimeona uwezo wao baada ya kucheza nao,"amesema Baraza nakuongeza kuwa.

"Ukikutana na timu ambayo wachezaji wanajiamini na wanacheza kwa kuonana basi hiyo ni hatari zaidi, siku hiyo niliona Simba wanacheza pasi, utulivu na kutumia mbinu zaidi, jambo litakalowasaidia wanakoelekea kimataifa,"amesema Baraza.

Mbali na kuiuzungumzia Simba kimataifa, amesema kwa upande wao wanajipanga kuhakikisha mechi zinazofuata wanafanya vyema ili kuanza kujiweka kwenye mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi.