Bao la kujifunga la Jones laimaliza Man United

Muktasari:

  • Jinamizi la kujifunga kwa mabeki wa timu ya Manchester United limeendelea tena baada ya jana usiku Phil Jones kujifunga wakati akiokoa hivyo kuizawadia Valencia bao la pili lililowatoa wageni mchezoni na kupoteza mchezo huo wa mwisho wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakifungwa 2-1 hivyo kumaliza katika nafasi ya pili KUndi H

Valencia, Hispania. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, amesema kilichosababisha wapoteze mchezo wao dhidi ya Valencia kwenye Uwanja wa Mestalla jana usiku ni bao la kujifunga la beki Phil Jones.

Huo ulikuwa mchezo wa mwisho wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu wa 2018/19 ambapo United ilihitaji kushinda ili kukaa kileleni na kukwepa kupangiwa timu vigogo katika hatua ya 16 bora.

Katika mchezo huo timu hizo zilikwenda mapumziko wenyeji wakiongoza kwa bao 1-0, lililofungwa na Carlos Soler dakika ya 17, ingawa Man United ilitawala mchezo huo lakini washambuliaji wake wakiongozwa na Romelu Lukaku hawakuwa makini.

Mourinho ambaye kabla ya mchezo huo alimrushia maneno kiungo wake Paul Pogba, akimtaka kucheza kwa makini na kujituma alisema kuwa wakati wa mapumziko aliwaambia vijana wake kwamba ubunifu ulipungua hivyo watulie.

Katika mchezo huo Pogba alionyesha uwezo mkubwa akishirikiana na Marouane Fellaini, walitawala eneo la kiungo hata hivyo hawakuweza kupenyeza mipira kwa washambuliaji wao.

Kama sio kuingia kwa shujaa wao katika siku za hivi karibuni Marcus Rashfod akitokea benchi na kuifungia Man United bao la kufutia machozi zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo huo kumalizika timu hiyo ingetoka kapa.

 “Tulicheza vizuri na tuliutawala mchezo wakati wa mapumziko niliwaambia kuwa wakatafute bao la kusawazisha hata hivyo Phil Jones akawatoa mchezoni baada ya kujifunga katika dakika ya pili ya kipindi cha pili,” alisema.

Mourinho alisema matokeo hayo ni changamoto kwao na kwamba wanatakiwa kubadilika katika michezo ijayo, ikiwa wanataka mafanikio ya uwanjani.

Iwapo Man United wangeshinda mchezo huo wangeongoza kundi hilo kwani Juventus iliyokuwa kileleni nayo ilipoteza mchezo wa jana ikifungwa 2-1 na vibonde wa kundi hilo Young Boys ya Uswisi.

Mourinho alikiri kuwa vijana wake hawakuwa makini kuzitumia nafasi ndiyo maana wakashindwa na timu hiyo inayoshika nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi ya Hispania, ambayo pamoja na ushindi huo itashiriki mashindano ya Europa Ligi.

Mourinho alisema anadhani kilichochangia wao kupoteza mchezo huo ni fikra kwa wachezaji kwamba wameshafuzu hivyo kutoutilia maanani mchezo huo ambao kwa upande wake anaamini ulikuwa muhimu kushinda.

Hata hivyo alionya matokeio ya ushindi huipa timu kujiamini zaidi katika michezo iliyo mbele yao hivyo atazungumza na vijana wake ili kukomesha hilo lisijirudie tena katika mechi zijazo.