Bado nyie na mwarabu tu

ILE furaha iliyokuwa imetoweka usoni mwa mashabiki wa Simba tangu timu yake ifumuliwe mabao 5-0 katika mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika, imerejea tena.

Ndio, kikosi cha wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya CAF jana walirejea kwa kishindo kwenye mechi zake za Ligi Kuu Bara kwa kuifumua Mwadui mabao ....na kuwafanya mashabiki wake kuimba ‘bado nyie...Bado Waarabu’ (wakimaanisha Yanga na Al Ahly).

Simba inatarajiwa kucheza na Waarabu Jumanne ijayo katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa, kabla ya kuvaana na Yanga kwenye mchezo mwingine wa marudiano wa Ligi Kuu.

Katika mechi yao kwanza ya Watani, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu, lakini Yanga walikuwa wakipiga kelele na kuwanyamazisha wenzao kutokana na matokeo iliyokuwa ikipata kwenye mechi zao za Ligi Kuu huku, Simba ikiyumba kimataifa.

Simba ilifumuliwa mabao 5-0 na AS Vita ya DR Congo mjini Kinshasa kisha kulala tena kwa idadi kama hiyo mbele ya Al Ahly wiki iliyopita na kuwanyong’onyesha mashabiki wao.

Hata hivyo mabao ya Meddie Kagere aliyevunja ukame wa mabao tangu alipofunga bao lake la mwisho Novemba 3 mwaka jana na mengine ya Mzamiru Yassin na John Bocco, yalirejesha furaha ya Wanamsimbazi ambao walisahau machungu yote ya nyuma na kuimba kwa furaha.

Kocha Patrick Aussems alifanya mabadiliko katika kikosi chake kama iliyoripotiwa na Gazeti la Mwanaspoti la jana Alhamisi, akiwaanzisha Zana Coulibaly, Mohammed Hussein, Paul Bukaba, Mzamiru Yassim na Haruna Niyonzima na kuwachomoa kina Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Jonas Mkude na Emmanuel Okwi walioanzia benchi.

Kagere alifunga bao lake dakika ya 21, akipokea krosi safi kutoka kwa kiungo fundi Cletus Chama kabla ya Mzamiru kuongeza la pili dakika ya 26 akipokea pasi ya kifua ya Bocco ambaye dakika tatu baadae alifunga bao la tatu kwa kichwa akimalizia krosi ya Niyonzima.

Mwadui walianza mchezo huo kwa kasi kwa kuizima Simba eneo la kati kwa dakika 20 za awali kabla ya bao la Kagere waliyemweke mtego wa kuotea kuwatibulia kwa bao la kichwa, likiwa bao lake la nane msimu huu na la kwanza tangu afunge mara ya mjini Tanga.

Kipindi cha pili Simba ilionekana kupunguza makali na hasa baada ya mabadiliko ya kuwatoa Mzamiru, Kagere, Chama na kuwaingiza Okwi, Mkude na Salamba, huku Mwadui walionekana kusaka angalau bao la kufutia machozi lakini ukuta wa Simba ikikuwa kikwazo kwao. Katika mchezo wao wa kwanza msimu huu, Mwadui ililala mabao 3-1 nyumbani na kipigo cha jana kimeifanya msimu huu kugawa alama sita kwa Wekundu wa Msimbazi ambao wanaanza maandilizi ya kuvaana na Al Ahly.

Kwa ushindi huo, Simba imechupa kutoka nafasi ya tano mpaka ya tatu ikifikisha alama 36 ikilingana na LIpuli, ila ikibebwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa baada ya mechi 15, huku wapinzani wao wakiganda nafasi yao ya 16 ikiwa na alama 24 kwa mechi zao 25. Pointi ilizonazo Simba ni pungufu 19 ilizonazo watani wao Yanga waliopo kileleni na alama 55 zilizotokana na mechi 21. Yanga wikiendi hii itavaana na JKT Tanzania kabla ya kuisubiri Yanga Februari 16.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo mapema jioni, Coastal Union ililazimishwa sare nyingine ya bao 1-1 na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga ambapo wageni walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya 37 kupitia William Patrick kabla ya wenyeji kuchomoa dadkika ya 65 lililofungwa na Raizin Hafidh.