Arusha Utd waiwahi Serengeti Boys

UJANJA kuwahi na kupata vilevile. Arusha United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kusikia timu ya taifa ya vijana U17, Serengeti Boys ipo kambini jijini hapa, fasta ikaamua kuchangamkia fursa kwa kuomba kukipiga nao mechi ya kirafiki.

Serengeti imepiga kambi Arusha kujiandaa na ushiriki wao wa michuano maalum ya UEFA Assist itakayofanyika Uturuki mapema mwezi ujao ikiwa sehemu ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana U17 itakayofanyika nchini Tanzania kati ya Aprili 14-28.

Timu hiyo iliamua kukimbilia Arusha ili kuizoea hali ya ubaridi kwani Uturuki wanakoenda kushiriki michuano hiyo nako kwa sasa kuna baridi tofauti na hali ya joto iliyokuwapo jijini Dar es Salaam ilipowekwa kambi ya awali.

Lakini kuwepo kwa timu hiyo ya vijana jijini hapa kumewafanya Wana Utalii, Arusha United kuchangamka kwa kuwaomba mechi ya kirafiki itakayopigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kocha Msaidizi wa Arusha, Masoud Juma alisema wamefikia hatua ya kuomba mchezo huo mara baada ya kuona ratiba ya FDL imesimama kwa muda huu kupisha michuano ya Kombe la FA ikataopigwa kuanzia leo mpaka Jumatatu ijayo.

“Wiki hii hatuna mechi za Ligi, hivyo tumeona ili kuwaacha wachezaji kwa wiki kama mbili wapumzike tu inaweza kupunguza makali yao, hivyo ujio wa Serengeti Boys tukaona ndiyo fursa kwetu ya kuwaomba kucheza nao mechi ya kirafiki kuwaweka vijana wawe fiti,” alisema Juma.

Aliongeza katika mchezo huo wanatarajia kunufaika mambo mengi ikiwemo mbinu za mchezo huo hasa ukabaji, ushambuliaji na hata ufungaji ambayo wanaamini itawasaidia katika programu zao za mazoezi na mashindano katika mechi zinazofuata.

“Unajua vijana hawa tayari wako ngazi ya juu ya kisoka kutokana na kushiriki mashindano mbali mbali makubwa ya kimataifa, hivyo kupata nafasi tu ya kuwa nao uwanja mmoja ni faida kwetu kuvuna walichonacho.”