Arsenal kwa Ancelotti ni buree

Muktasari:

Ancelotti ameelezwa kwamba anajiandaa kutua England ndani ya saa 24 zijazo kwenda kuzungumza na Toffees ili kuchukua mikoba ya timu hiyo yenye maskani yake Goodison Park. Lakini, Arsenal nao wanapambana kunasa huduma yake.

LONDON, ENGLAND . ARSENAL mpo? Ripoti za kutoka Italia zinafichua kwamba Arsenal watamchukua bure bila ya kulipa fidia yoyote kwa Napoli Mtaliano Carlo Ancelotti kama watahitaji aende akawe kocha wao mpya.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 60 alifutwa kazi Napoli wiki hii licha ya kuongoza timu hiyo kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arsenal wamekuwa wakihusishwa na kocha huyo kwamba atakwenda kuchukua mikoba baada ya kuachana na Unai Emery, lakini Everton nao wanaripotiwa kwamba wapo sokoni kusaka kocha mwenye uzoefu baada ya kuachana na Marco Silva.
Ancelotti ameelezwa kwamba anajiandaa kutua England ndani ya saa 24 zijazo kwenda kuzungumza na Toffees ili kuchukua mikoba ya timu hiyo yenye maskani yake Goodison Park. Lakini, Arsenal nao wanapambana kunasa huduma yake.
Kwa mujibu wa Daily Mail, Arsenal wameonekana kuwa na mipango na kocha huyo wa zamani wa Chelsea akachukua mikoba ya timu hiyo baada ya sasa kuwa chini ya Freddie Ljungberg katika kipindi cha mpito. Arsenal wameambiwa kwamba hawatalipa fidia yoyote ya kumchukua Ancelotti, ambaye ataendelea kupokea mishahara kutoka Napoli hadi mwishoni mwa msimu au hadi hapo atakapopata kazi mpya. Kesho Jumapili, Arsenal watakuwa na mtihani mzito kwenye Ligi Kuu England watakapowakabili Manchester City uwanjani Emirates.