Andrew Vincent ‘Dante’ ajitosa mazima Simba

Muktasari:

  • ANDREW Vincent Dante wa Yanga anajua wazi klabu yake haina chao katika anga la kimataifa na fasta anaamua kujitosa Msimbazi kwa nia ya kutaka kuisaidia klabu hiyo itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ifanye vizuri CAF.

NYOTA wa Simba, Emmanuel Okwi, Middie Kagere na John Bocco wanaijua vyema kazi ya beki ya kati ya Yanga hasa Andrew Vincent ‘Dante’, lakini sasa unaambiwa beki hiyo ameamua kujitosa mazima Msimbazi.

Akiwa na uchungu wa klabu yake kushindwa kushiriki michuano ya kimataifa kwa msimu huu, Dante ameamua kuwavaa nyota hao wa Simba na kudai wao ndio waliobeba tumaini na watani zao katika michuano ya CAF msimu huu.

Dante alisema wakali hao ndio watakaoamua hatma ya Simba katika mechi zao za raundi ya awali dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini watakaovaana nao kwanza Novemba 27-29 kabla ya kurudiana nao wiki moja baadaye.

Dante alisema kwa uzoefu walionao safu ya mbele ya Simba ambao ni bandika bandua kwenye kikosi chao na timu zao za Taifa, wanapaswa kuuthibitishia umma kuwa wapo matawi ya juu kwa kuibeba klabu yao CAF.

“Safu ya Simba ina watu walio tayari wameonyesha wao ni kina nani katika ligi, hivyo lazima watambue wana deni mbele ya mashabiki wao kwa kuhakikisha wanaibeba timu yao katika mechi za CAF, wao ndio kila kitu,” alisema.

Dante pia aliwageukia nyota wa Simba wanaocheza katika nafasi nyingine nao kutimiza majukumu yao uwanjani ili kuipaisha Simba kimataifa sambamba na kutengeneza majina yao katika anga hizo.

BAHANUZI AIBUKA

Katika hatua nyingine, straika wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi aliyekuwa kimya kwa muda mrefu ameibuka na kueleza anavyofuatilia kila kinachoendelea katika soka la Bongo na kuwashtua Simba wajipange kimataifa.

Bahanuzi alisema Simba waitumie vyema nafasi waliopata anga za kimataifa hasa kwa wachezaji ambao majina yao yamepelekwa CAF kwa ajili ya Ligi ya mabingwa Afrika.

“Mimi nazikumbuka nafasi nilizopata enzi nikiwa Yanga, vivyo hivyo nawasihi wachezaji wa Simba, kutumia vyema kuvitangaza vipaji vyao ama kufanya biashara nzuri ya soka dhidi ya timu wanazocheza nazo,” alisema.

Naye aliyekuwa Rais wa TFF, Muhidini Ndolanga alisema kuelekea michuano ya kimataifa ya Afrika Simba na Mtibwa watakaoshiriki Kombe la Shirikisho kutakiwa kuonyesha ukomavu wao, nidhamu na kutambua thamani ya kushiriki kwao. “Simba sio wageni na hiyo michuano ifikie hatua kwa wachezaji kuthamini sana nafasi wanazozipata, wawe wanajisikia vibaya pindi ikitokea wanafanya ovyo na wenzao wanasonga mbele, Tanzania sasa tunahitaji kusonga mbele.

“Ndio maana kila wakati nazungumza kwamba hakuna mafanikio ya njia fupi, soka ni sayansi lazima hizi Simba na Yanga zifikie hatua ziwe mfano kwa hizi klabu nyingine wanazoshiriki nazo ligi kuu, pia wafanye kitu cha tofauti msimu huu bila kuwasahau Mtibwa Sugar,” alisema.