Akili za mkulima zinavyozalisha mabao ya Simba

Friday April 5 2019

 

By CHARLES ABEL

HAKUNA sababu ya kushangaa matokeo mazuri ambayo Simba imeyapata ndani ya uwanja kwenye mashindano tofauti inayoshiriki kwa sasa.

Ni matokeo ya uwekezaji na uvumilivu ilioufanya kama vile maisha ya mtu anayefanya shughuli za kilimo.

Uvumilivu wa mkulima mara kwa mara humfanya achelewe kunufaika lakini pindi muda sahihi wa mavuno unapofika, sura yake ni lazima ionyeshe tabasamu. Baada ya tabu za kuandaa mashamba, kupanda na kupalilia wakati wa mavuno ndicho kipindi ambacho mkulima huwa hana kazi kubwa zaidi ya kunufaika na jasho alilomwaga siku za mwanzoni.

Simba kesho itacheza mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Imestahili kufika kwenye hatua hiyo iliyopo na sio vibaya kusema hakukuwa na njia ya mkato kwao hadi inafika hapo ilipo ni kutokana na maandalizi iliyoyafanya mwanzoni mwa msimu.

Kabla ya msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuanza, lengo la Simba lilikuwa ni kufika hatua ya makundi ya mashindano hayo kutokana na maandalizi iliyoyafanya lakini hatimaye imevuka lengo na kufika robo fainali.

Hata ikitokea ikitolewa na TP Mazembe, bado Simba inapaswa kupewa pongezi badala ya kubezwa. Lengo lake ilishalivuka na kufuzu robo fainali ilikuwa ni bonasi tu. Wanasema siku zote hakuna ziada mbovu.

Lakini hata kama Simba ingeishia hatua ya makundi, bado hilo lisingetokea kwa bahati mbaya. Yangekuwa ni matokeo ya uwekezaji na subira ambayo tunaona sasa inalipa hadi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kabla ya msimu huu kuanza, Simba iliweka kambi ya maandalizi Uturuki ambako pia ilicheza mechi kadhaa za kirafiki. Kambi za namna hii siku zote zimekuwa na matokeo chanya kwa timu kwani ndizo zinatumiwa na benchi la ufundi kuandaa mipango ya kiufundi na kimbinu pamoja na kutengeneza uelewano wa kitimu.

Sio vibaya kwa timu kuweka kambi ya kujiandaa na msimu hapa nchini, lakini ni ukweli usiofichika kwamba zile za nje ya nchi kama ilivyo kambi ya Uturuki zina faida kubwa kwa sababu wenzetu wana miundombinu ya kisasa na inayojitosheleza ambayo inazifanya timu zijiandae vizuri tofauti na hapa nyumbani.

Lakini pia kambi za nje ya nchi zinasaidia wachezaji kuwa sawa kisaikolojia pamoja na kupata utulivu wa hali ya juu ambao huwafanya wajiandae vyema kabla ya msimu kuanza.

Na ushahidi wa hilo uko wazi jinsi timu mbalimbali ambazo ziliweka kambi nje ya nchi zao zinafanya vizuri kwa sasa katika mashindano mbalimbali ambayo zinashiriki.

Kule Uturuki, Simba ilikuwa pamoja na timu za Itihad De Tanger ya Morocco pamoja na JS Saoura ya Algeria. JS Saoura iliingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa Ittihad de Tanger kwenye raundi ya kwanza lakini Tanger ilipoangukia kwenye Kombe la Shirikisho ilitinga hatua ya makundi.

Mwaka 2014 Yanga iliweka kambi (Pre Season) Uturuki, ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu katika msimu wa 2014/2015, 2015/2016 hadi 2016/2017 pamoja na Kombe la FA.

Hiyo haikutosha kwani mwaka uliofuata, Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuiondoa Sagrada Esperanca ya Angola kwenye hatua ya mwisho ya mtoano. Lakini pia mbali na kuliboresha benchi lake la ufundi kwa kumleta Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems, Simba ilimuajiri mtaalamu aliyebobea katika kujenga stamina na ufiti wa wachezaji, Adel Zrane kutoka Tunisia.

Ni huyo Zrane ambaye leo hii amewafanya wachezaji wa Simba kuwa na pumzi na stamina ya kutosha kwa dakika zote 90 za mchezo kulinganisha na siku za nyuma ambazo walikuwa wanachoka mapema.

Kiufupi soka la kisasa linaendeshwa kisayansi na kile unachokipanda ndicho unachokuja kukivuna.Tunapowaona kina John Bocco, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Clatous Chama wanazitesa timu pinzani kwenye mashindano ya ndani na nje, tunapaswa kukumbuka maandalizi mazuri ambayo Simba iliyafanya mwanzoni mwa msimu.

Advertisement