Ajibu, Bocco wapewa ramani

Friday September 14 2018

 

By OLIPA ASSA

OLIPA ASSA


KAMA Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude na nyota wengine kadhaa wanaong’ara kwa sasa nchini watazingatia mchoro wa ramani waliopewa na kiraka wa zamani wa kimataifa, basi lazima watusue anga za kimataifa.

Unajua wamepewa mchongo gani? Nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Mtwa Kihwelo ‘Dally Kimoko’, amewaambia ukweli mafundi hao wa soka akiwamo John Bocco, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Aishi Manula na Juma Abdul wasikubali soka lao liishie Tanzania.

Mtwa alisema wachezaji hao wasijione wamefanikiwa vya kutosha badala yake wawe na kiu ya kufuata nyayo za kina Mbwana Samatta anayekipiga Ubelgiji, Abdi Banda (Afrika Kusini), Saimon Msuva (Morocco) na Hassan Kessy (Zambia).

“Tuwe wakweli ipo tofauti ya thamani ya mchezaji anayecheza nje na ndani, ndio maana wakija kina Samatta, Msuva, Banda, Thomas Ulimwengu na Kessy kuonekana kitu tofauti katika timu ya taifa, hilo lingekuwa somo tosha kwa akina Ajib, Bocco, Manula, Mkude na wenzake kupanua wigo wao wa kutoka nje.

“Unajua hata ungecheza kwa kiwango kikubwa soka la ndani, ukashindwa kwenda nje kwa miaka ya sasa unapotundika daruga unaonekana bure kabisa, wachezaji, wachangamke sasa, fursa hii.”