Solskjaer ajitetea usajili Man United

Muktasari:

Katika hatua nyingine, kocha Solskjaer ameamua kumfanya Anthony Martial kuwa mshambuliaji wake kiongozi msimu huu baada ya kumkabidhi jezi yenye namba 9 baada ya kumpiga bei Romelu Lukaku.

MANCHESTER, ENGLAND . KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema hakukuwa na shida yoyote ya pesa wakati wa usajili na kwamba kilichotokea hawakuona mchezaji sahihi wa kusajili zaidi.
Man United ilifanya usajili wa wachezaji watatu tu kwenye dirisha la majira ya kiangazi, ilipowanasa Harry Maguire, Aaron Wan-Bissaka na Daniel James kwa zaidi ya Pauni 145 milioni.
Alipoulizwa kama pesa ilikuwa kikwazo cha kushindwa kufanya usajili zaidi, Solskjaer alisema: "Pesa ilikuwapo ya kutosha tu na ingetumika kama kungekuwa na wachezaji sahihi.
"Hapa halikuwa suala la kusajili tu kwa ajili ya shida ya sasa, lilikuwa suala la kujenga timu kwa muda mrefu. Sio suala la kubadili mipango pindi unapoona umekwamba. Nimefurahishwa na wachezaji hawa watatu tuliosajili."
Katika hatua nyingine, kocha Solskjaer ameamua kumfanya Anthony Martial kuwa mshambuliaji wake kiongozi msimu huu baada ya kumkabidhi jezi yenye namba 9 baada ya kumpiga bei Romelu Lukaku.
Kocha huyo amesema kwamba anaamini kwa kiasi kikubwa kwamba Martial atamaliza tatizo la kufunga kwenye kikosi hicho na kuwafanya kutokuwa na ukame wa mabao kama inavyodhaniwa kwa sasa baada ya Lukaku kutimkia Inter Milan. Kocha huyo anaamini Martial ni mtu sahihi wa kucheza katikati na hapo kwenye fowadi ataunda pacha na Marcus Rashford. Katika kipindi ambacho Lukaku alikuwa kwenye kikosi hicho, Martial alikuwa akicheza upande wa kushoto.
Mashabiki wa Man United wanafurahia kwa timu hiyo kumpiga chini Lukaku, ambaye katika kipindi cha misimu miwili amefunga mabao 42 akicheza mshambuliaji wa kati. Ndani ya kipindi hicho, Rashford amefunga mabao 26 na Martial mabao 23, lakini tofauti ni kwamba wawili hao walikuwa wakishambulia kitokea pembeni.
Solskjaer alisema: “Sawa, Rom amekuwa na rekodi nzuri hasa anapocheza mshambuliaji wa kati. Lakini, nina hakika tutafunga mabao ya kutosha tu kutoka kwa Anthony Martial, Marcus Rashford, Dan James na Jesse Lingard."