Real hawajui wamefungwaje 3-0

Muktasari:

  •  Timu ya Real Madrid jana ilipoteza mchezo ikiwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Santiago Bernabeu ilipofungwa mabao 3-0 na CSKA Moscow ya Russia kikiwa kipigo kikubwa cha kwanza cha Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu Santiago Solari apewe jukumu la ukocha mwezi uliopita

Madrid, Hispania. Kocha wa Real Madrid, Santiago Solari, amesema hajui ilikuwaje wakafungwa mabao 3-0 na CSKA Moscow timu inayoburuza mkia katika kundi G wakiwa nyumbani Santiago Bernabeu.

Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza kikubwa kwa Madrid, bingwa mtetezi wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, tangu Solari amepewa jukumu hilo la uongozi na bahati pekee waliyonayo ni kwamba waliingia katika mchezo huo wakiwa wameshafuzu hatua ya 16 bora.

Real ikiwa na kikosi kamili wakiwemo Karim Benzema, Marcelo, Marco Asensio, Isco, Bale na kipa mahiri wa Ubelgiji, Thibaut Courtois, walipotezwa kabisa na wageni wao kiasi kwamba wakawa kama wanacheza ugenini.

“Kwa kweli tumecheza kwa kiwango duni kabisa leo tulistahili kufungwa, tulianza mchezo vizuri katika dakika 15 za kwanza lakini tulizembea na kujikuta tukifungwa mabao mawili ndani ya muda mfupi ambayo yalituchanganya,” alisema.

Katika mchezo huo Fedor Chalov ndiye aliyefungua pazia la mabao katika dakika ya 37 kabla ya Georgi Schennikov kuongeza la pili dakika ya 43 na kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili wenyeji walipambana kusaka mabao ya kusawazisah bila mafanikio na kadiri muda ulivyosonga ndivyo walivyozidi kupoteza umakini uwanjani.

Mchezaji Arnor Sigurdsson ndiye aliyewalazimisha baadhi ya mashabiki wa Real kuondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika baada ya kufunga bao la tatu katika dakika ya 73.

Hata hivyo Real imetinga 16 bora ikiongoza kundi huku AS Roma ikichukua nafasi ya pili licha ya kufungwa 2-1 na Viktoria Plzen ambayo iliweza kujikatia tiketi ya kucheza Europa Ligi, huku CSKA Moscow ikimaliza ya mwisho.

Solari aliamua kumtoa Benzema aliyekuwa akipoteza nafasi za kufunga mabao na kumuingiza Gareth Bale mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo na kocha huyo alitoka uwanjani akionekana amekasirika.

Matokeo yote ya mechi za Ligi hiyo zilizochezwa jana usiku ni, Real Madrid 0 CSKA Moscow 3, Viktoria Plzen 2 Roma 1, Ajax 3  Bayern Munich 3, Benfica 1 AEK Athens 0, Man City 2 Hoffenheim 1, Shakhtar Donetsk 1 Lyon 1, Valencia 2 Man Utd 1 na   Young Boys 2 Juventus 1.