Mbeya City wadai kuimarika, hawashuki daraja

Muktasari:

Mbeya City ndio timu ya kwanza kutinga hatua ya 16 bora kwa kuitoa Polisi Tanzania michezo mingine nane inatarajiwa kuchezwa kesho kwenye viwanja mbalimbali.

BAADA ya kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la FA kipa wa Mbeya City, Aron Kalambo amesema haikuwa kazi rahisi wao kutinga hatua hiyo na kuweka wazi kuwa imewapa mwanga kuwa kikosi chao kinaimarika kadri muda unavyozidi kwenda.

Mbeya City imetinga hatua hiyo kwa mikwaju ya penati 3-1 baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 kwa matokeo hayo City anasubiri mshindi kati ya Ndanda FC na Dodoma.

Kalambo amesema wana kikosi kipya ambacho ni kama kinasukwa upya walikutana na timu ambayo ina wachezaji wengi wazoefu hivyo walipambana kuhakikisha wanapata nafasi ya kuendelea wanamshukuru Mungu kupita hatua hiyo.

"Unajua sisi ndio kwanza tunasuka kikosi lakini kadri muda unavyozidi kwenda kuna mabadiliko makubwa yanaonekana kama tutaendeleza juhudi hizi basi hata kwenye ligi tunaweza kukwepa kushuka daraja kwa michezo iliyobaki,"

"Polisi ni timu ngumu na nzuri tulipambana sana kupata matokeo hadi dakika 90 tulikuwa nguvu sawa kila timu ilipata nafasi ya kufunga bao 1-1 mikwaju ya penalti ilitubeba ubora wetu ulionekana tofauti na michezo mingine," alisema.

Mbeya City kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara inashika nafasi ya 17 wakiwa na pointi 13, nafasi ambayo kwao ni mbaya kwani wasipopambana wanaweza kushuka daraja.