Mbao FC yawakana Yanga sakata la kumtimua Benitez

Muktasari:

Njashi aliongeza kuwa kwa sasa wameanza mazungumzo na baadhi ya Makocha lakini wote wanatoka hapa hapa Tanzania hivyo watamtangaza siku za usoni na atakua Kocha Mkuu sio Msaidizi kama alivyokua Bushiri.

MWANZA. WAKATI huko mtaani baadhi ya wadau wa Mbao FC wakisema kuwa kichapo walichopata timu yao kutoka kwa Yanga cha 2-1 ndicho kimehusika kumfukuza Kocha Ally Bushiri, Mwenyekiti wa timu hiyo Solly Njashi amesema Yanga hawahusiki katika sakata hilo.

Timu ya Mbao FC yenye maskani yake Ilemela Mwanza inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 36 katika michezo 30 waliyoshuka dimbani.

Akizungumza na Mwanaspoti Mwenyekiti huyo alisema kuwa matokeo mabovu waliyopata timu yao tangu Kocha Msaidizi Bushiri apewe mikoba ndiyo imepelekea kumfungashia virago na sio mechi waliyodundwa na Yanga hapa Kirumba.

"Mechi moja haiwezi kumpima uwezo wa Mwalimu, kufungwa na Yanga sio tatizo, swala linakuja tangu Kocha Mkuu Amri Said aondoke tumecheza mechi 13 na tumeshinda tatu na kutoa sare tatu hivyo kwa mwenendo huo tungemvumilia?" alisema Njashi.

Alisema Mbao FC imeporomoka kutoka nafasi ya sita mpaka 15 ni kutokana na matokeo hayo mabaya waliyopata walipokua na Kocha huyo hivyo ili kuinusuru timu ni  vyema kufanya maamuzi magumu mapema.

Njashi aliongeza kuwa kwa sasa wameanza mazungumzo na baadhi ya Makocha lakini wote wanatoka hapa hapa Tanzania hivyo watamtangaza siku za usoni na atakua Kocha Mkuu sio Msaidizi kama alivyokua Bushiri.

Aliwaomba Mashabiki na Wadau wa timu hiyo wasikate tamaa wala wasiwe na wasiwasi katika kipindi hiki cha mpito kwani Viongozi wao wana mikakati  kambambe ya kuhakikisha timu inafanya vizuri msimu huu kuliko msimu uliopita.

"Najua ni ngumu kuondoa wasiwasi  miungoni mwa wana Mbao, na hili limetokana na matokeo mabovu tuliyopata, ila nina imani baada ya kuja kwa Kocha mpya mambo yataenda sawa hivyo watarejesha furaha yao tena aliyoianzisha Amri Said " alisema Mwenyekiti huyo.