Huu mziki wa makipa Yanga acha kabisa

Thursday October 01 2020
yangaa pic

KOCHA wa makipa wa Yanga, Vladimir Niyokuru amesema kiwango kilichooneshwa na makipa wake katika mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM uliochezwa jana Septemba 30 kwenye Uwanja wa Azam Complex,kilikuwa ni kikubwa na wamezidi kuimarika, tofauti na alipoanza nao mwanzoni wa msimu.

 Niyokuru amesema kinachohitajika kwao sasa ni muendelezo wa kile ambacho wameanza tokea mwanzoni mwa msimu ambapo wameruhusu bao moja katika michezo saba ya michuano yote.

 "Siwezi kumtaja kipa mmoja kama ndio amecheza vizuri lakini kwa upande wangu wote walionesha kiwango kikubwa na sio kwenye mchezo huo tu, hata kwenye zile nyingine zilizopita,"alisema.

 Akizungumzia mchezo dhidi ya Simba unaotarajiwa kupigwa Oktoba, 18, Niyokuru alisema huwa anawandaa wachezaji wake kwa michezo yote na sio Simba pekee.

 "Kuna timu 18, kwenye Ligi Kuu, mimi huwa nawaandaa makipa na kuwaambia wacheze vizuri kwenye kila mechi, hivyo sihitaji kuwapa presha yakuanza kuwaandaa dhidi ya mchezo huo wakati tuna mechi Jumamosi Oktoba, 3, dhidi ya Coastal Union,"alisema.

 Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 , ambayo yote yalifungwa na kiungo wake kutoka Congo, Mukoko Tonombe dakika ya 11 na 31.

Advertisement

 

Advertisement