Mashabiki Mwanza wanataka kumwona Molinga, Balinya

Muktasari:

Yanga itacheza michezo miwili ya kirafiki Jijini hapa dhidi ya Pamba FC na Toto Afrikans kwaajili ya maandalizi ya mchezo wa Kimataifa dhidi ya Zesco United utaopigwa Jijini Dar-es-salaam.

MASHABIKI wa Yanga jijini hapa wamejipanga kujitokeza kwa wingi kesho Jumamosi kushuhudia mechi ya kirafiki dhidi ya Pamba FC lakini kiu yao kubwa ni kuwaona nyota wao wapya wakiwemo David Molinga na Juma Balinya.
Mechi hiyo ya kujipima nguvu itachezwa uwanja wa CCM Kirumba ambapo Yanga inajiandaa kucheza mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia wakati Pamba wao wanajiandaa kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa matawi ya Yanga jijini hapa wamesema mashabiki wamepanga kuujaza uwanja huo ili kuwashuhudia nyota wao hasa Molinga, Balinya na wengine ambao hawajawahi kuwaona .
Katibu wa Yanga tawi la Pasiansi, Emmanuel Babu amesema usajili uliofanywa msimu huu umewapa nguvu ya kuamini watafanya vizuri katika mashindano yote huku nyota hao wakiongeza chachu kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi.
"Hao akina Molinga na Balinya tumezoea kuwaona kwenye televisheni tu, mashabiki wa hapa kwetu wanataka kuwashuhudia hivyo wamejipanga vizuri kwenda Kirumba kuwashuhudia na kuwasapoti," amesema Babu
Katibu wa Matawi ya Yanga Mkoa wa Mwanza, Muhando Madega amesema maandalizi kuelekea pambano hilo yapo vizuri hivyo mashabiki wametakiwa kwenda kwa wingi kwani watapata pia fursa ya kupiga picha na mastaa wao.