Emre Can sasa anajuta tu Juventus

Muktasari:

Kocha Sarri ameamua kumpiga chini Can kwenye kikosi chake kwa mechi za makundi, ambapo timu hiyo imepangwa kuzikabili Atletico Madrid, Bayer Leverkusen na Lokomotiv Moscow.

TURIN, ITALIA. KIUNGO, Emre Can amefyumu na kukasirika baada ya Juventus kumpiga chini kwenye kikosi chao kitakachocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Kiungo huyo wa Kijerumani aliachana na Liverpool kwenda kuungana na Juventus kwa uhamisho wa bure Juni 2018 kwa sababu alitaka kwenda kucheza kwenye klabu kubwa zaidi. Kwenye kikosi cha Juve, amecheza mechi 37 msimu uliopita, lakini sasa amekuwa hana nafasi kwenye timu baada ya ujio wa viungo Aaron Ramsey na Adrien Rabiot msimu huu, huku kikosi kikiwa chini ya kocha mpya, Maurizio Sarri.
Kocha Sarri ameamua kumpiga chini Can kwenye kikosi chake kwa mechi za makundi, ambapo timu hiyo imepangwa kuzikabili Atletico Madrid, Bayer Leverkusen na Lokomotiv Moscow.
Can alisema: "Nimeshtusha na nimekasirika. Wiki iliyopita, klabu ilinipa ahadi nyingi. Majuzi kocha ananiita na kuniambia kwamba sipo kwenye kikosi tena akitumia muda mfupi tu kunieleza, hata dakika haijafika. Nashindwa kuelezea, kwa sababu sijapewa sababu yoyote.
"Mimi na wakala wangu tulizungumza na timu nyingine kwenye kipindi cha usajili, lakini baada ya kuzungumza na Juventus nikaamua kubaki. Kwangu mimi, moja ya sababu zilizonifanya nibaki ni kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kama ningefahamu hilo mapema, nisingebaki. Naomba niishie hapo, nitazungumza na klabu na wakala wangu."
Lakini, mashabiki wala hawajamwonea huduma kiungo huyo, huku mmoja akiandika kwenye Twitter: "Emre Can aliondoka Liverpool kwa sababu alijiona yeye ni mchezaji mkubwa na alitaka kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya. Miaka miwili baadaye, Liverpool wanachukua ubingwa wa Ulaya na kupoteza kwenye mechi ya fainali, Emre Can yeye hata kwenye kikosi cha Juventus hayumo. Gundu lako hilo."
Paris Saint-Germain na Bayern Munich zilionyesha dhamira ya kutaka huduma yake katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi huku Barcelona wakidaiwa kwamba walitaka kufanya dili la kubadilishana na Ivan Rakitic.