Wikiendi yamoto barani Ulaya
Muktasari:
- Ukiondoa mechi ya Bayern Munich na Borussia Dortmund pale Bundesliga pia kuna mechi ya Monaco na Marseille kule Ligue 1.
BARCELONA, HISPANIA: WIKIENDI ni yamoto na ligi mbalimbali zimerejea barani Ulaya. Utamu wa wiki hii unazidishwa na idadi kubwa ya mechi kubwa ambazo zitapigwa sehemu mbalimbali barani Ulaya.
Ukiondoa mechi ya Bayern Munich na Borussia Dortmund pale Bundesliga pia kuna mechi ya Monaco na Marseille kule Ligue 1.
Mbali ya mechi kubwa pia kuna suala la kuwania nafasi mbalimbali ambalo limekuwa habari ya mjini kwa sababu timu hazitofautiani sana alama. Hapa tumekuletea uchambuzi wa ligi nne bora barani Ulaya mbali ya EPL.
LA LIGA
Licha ya kuanza msimu vizuri, katika wiki za hivi karibuni Barcelona imeangusha pointi pointi nne baada ya kupoteza dhidi ya Real Sociedad kwa bao 1-0 kisha ikatoa sare ya bao 2-2 na Celta Vigo.
Matokeo hayo mabaya yamesababisha kupunguza utofauti wa pointi kati yao na Real Madrid.
Kwa sasa Barcelona ina pointi 34, huku Madrid ikiwa na 30 na hapo Barca inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mechi ukilinganisha na Madrid.
Mchezo wa kesho, dhidi ya Las Palmas, Barcelona itahitajika kushinda kwa gharama yoyote kwa sbabau ikipoteza na Madrid ikashinda dhidi ya Getafe keshokutwa, utofauti wa pointi itakuwa ni moja na kama ikishinda na kiporo chao Madrid itakuwa kuleleni kwa tofauti ya pointi mbili.
Hivyo mchezo huu ni muhimu kwa Barca ili kuendelea kuongoza msimamo.
Mchezo kati ya Barca na Las Palmas unatarajiwa kupigwa katika dimba la Nou Camp kuanzia saa 10:00 jioni, huku Madrid ikicheza kesho saa 12:15 jioni.
Atletico Madrid ambayo ipo katika nafasi ya tatu kwa pointi zao 29, yenyewe ikishinda mechi yao dhidi ya Valladolid inaweza kupanda na kushusha Madrid ikiwa haitoshinda mechi zake mbili zijazo.
Mchezo wa Atletico na Valladolid unatarajiwa kupigwa kesho kuanzia saa 5:00 usiku.
SERIE A
Huku kimenuka sana. Hakuna timu yoyote yenye uhakika wa nafasi yake. Utofauti wa pointi kutoka timu ya kinara Napoli yenye pointi 29 hadi nafasi ya tano ilipo Lazio yenye pointi 29, yoyote anaweza kupanda kileleni kwa kushinda mechi moja tu.
Napoli ambayo inaongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya nne za chini yake inahitaji kushinda kuendelea kushinda kwani kupoteza kwa namna yoyote au hata sare kunaweza kusababisha ijikute nafasi ya tano.
Ukiondoa timu hizi zilipo nafasi tano za juu, pia kuanzia nafasi ya sita ilipo Juventus hadi nafasi ya 11 ilipo Torino, mambo ni yaleyale tu. Ikiwa Torino itashinda mchezo wao dhidi ya Napili keshokutwa inaweza kupanda hadi nafasi ya saba.
Napol itakuwa uwanja kuvaana na Torino keshokutwa kuanzia saa 11:00 jioni muda sawa na Lazio itakapokutana na Parma, pia Inter itacheza na Fiorentina keshokutwa saa 2:00 usiku.
Kesho kutakuwa na mechi tatu ambapo AC Milan itacheza dhidi ya Empoli saa 2:00 usiku, Como na Monza saa 11:00 jioni na Bologna na Venezia saa 4:45 usiku.
BUNDESLIGA
Katika Bundesliga kesho ni siku ambayo mashabiki wengi walikuwa wakiisubiria. Ni miamba miwili itakuwa inaonyeshana ubavu ambao ni Bayern Munich na Borussia Dortmund.
Mchezo huo ambao utapigwa katika dimba la Signal Iduna Park kuanzia saa 2:30 usiku, utakuwa wa 136 kwa timu hizi kukutana katika michuano yote na Bayern ndio ina rekodi nzuri zaidi ikishinda 69, sare 31 na kufungwa 35.
Vilevile hii inaweza kuwa mechi ya kisasi kwa Bayern ambao mchezo wa mzunguko wapili dhidi ya Dortmund msimu uliopita ilichapika kwa 2-0 ikiwa ni moja ya sababu ya kulikosa taji la Bundesliga na kuchukuliwa na Bayer Leverkusen. Hivyo hii inaweza kuwa ni wakati wao wa kutaka kulipiza kisasi.
Licha ya kuanza vibaya ligi msimu huu, Dortmund imeendelea kutajwa kama moja kati ya timu shindani kwa Bayern na mchezo wao huu unatarajiwa kuvutia timu nyingi.
LIGUE 1
PSG itakuwa uwanjani kuvaana na Nantes saa 5:00 usiku katika mchezo ambao ikishinda itaendelea kujichimbia zaidi kileleni.
Mechi hii inaonekana kuwa muhimu zaidi kwa Nantes ambayo ikishinda inaweza kujiondoa katika nafasi 16 hadi ya 11 kwani itafikisha pointi 13,hata hivyo itategemea na matokeo ya timu nyingine zilizopo juu yao. Mchezo huu utapigwa katika dimba la Parc de Princess.
Keshokutwa ndio mambo yanatarajiwa kuchangamka zaidi kwani Monaco iliyopo nafasi yapili itaumana na Marseille iliyo nafasi ya tatu.
Timu hizi ambazo zimekuwa katika kiwango bora kwa msimu huu, zinaifukuzia PSG kimya kimya katika mbio za ubingwa na ikiwa Marseille inayofundishwa na Robert de Zerbi itashinda hapa itafikisha pointi sawa na Monaco(26) na kitakachoamua nani akae juu ya mwenzake ni mabao ya kufunga na kufungwa mechi hii itapigwa saa 4:45 usiku.