WAZEE WA KAZI: Makocha wanaoongoza kwa kubeba mataji mara nyingii

Saturday May 01 2021
wazee pic

LONDON, ENGLAND. PEP Guardiola na Manchester City wamebeba Kombe la Ligi msimu huu. Hilo ni taji la kwanza kwa miamba hiyo ya Etihad kwa msimu huu, huku wakipiga hesabu ya kunyakua mataji mengine mengi zaidi ili kumaliza msimu wao kibabe kabisa.

Kwenye Kombe la Ligi, vinara hao wa Ligi Kuu England waliichapa Tottenham Hotspur 1-0 uwanjani Wembley, hivyo kubeba kombe hilo kwa mara ya nne ndani ya misimu minne ya karibuni.

Mafanikio ya Mhispaniola Guardiola kwa kubeba taji hilo, limemfanya awe amebeba taji la tisa tangu alipojiunga na Man City majira ya kiangazi yam waka 2016.

Hadi kufika mwishoni wa msimu huu 2020/21, anaweza kuongeza mataji zaidi, akibeba taji lake la tatu la Ligi Kuu England na pengine anaweza kuipa Man City ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kikosi chake kwa sasa kufika hatua ya nusu fainali na usiku wa jana Jumatano walikuwa na shughuli pevu ya kuwakabili Paris Saint-Germain.

Lakini, bila ya kubeba taji la Ulaya msimu huu, mafanikio ya Guardiola, ambaye ubingwa wa michuano hiyo mara ya mwisho alibeba akiwa na Barcelona msimu wa 2008/09 hayatahesabika kuwa ya juu kwa sababu timu yake ya Man City kwa muda mrefu imekuwa ikiwekeza kwenye kikosi chake kwa ajili ya kunyakua taji hilo.

Baada ya ushindi wake dhidi ya Spurs, fundi huyo wa soka la kupiga pasi nyingi ‘tiki-taka’ umemfanya awe ameshinda mataji 30 na hivyo kushika nafasi ya tatu kwenye orodha ya makocha waliobeba mataji mengi zaidi kwenye soka la dunia.

Advertisement

Mwaka 2019, gazeti maarufu la Hispania la Marca lilitoa orodha ya makocha waliobeba mataji mengi, kati ya wanane, Guardiola alishika namba nne, lakini mwaka huu 2021 amepanda juu kwa nafasi moja.


8. Jose Mourinho (mataji 25)

Alijipachika jina la ‘Special One’ baada ya kuwapa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya FC Porto na kisha kunasa kibarua cha kwenda kuinoa Chelsea, mahali ambalo aliisaidia pia kufuta unyonge kwenye Ligi Kuu England. Jose Mourinho, ambaye Jumatatu iliyopita alifutwa kazi huko Tottenham Hotspur, ikiwa ni mwendelezo wake wa kutimliwa tu kwenye timu anazofanya kazi kwa miaka ya karibuni, alipita pia kwenye vikosi vya Inter Milan, Real Madrid na Manchester United na kote huko alisaidia timu hizo kunyakua mataji makubwa. Jambo hilo linamfanya Mreno huyo kuwa kwenye orodha ya makocha waliobeba mataji makubwa kwenye soka, akifanya hivyo mara 25.


7. Ottmar Hitzfeld (mataji 25)

Unamkumbuka Ottmar Hitzfeld? Alikuwa bonge la kocha kwenye mchezo huo wa soka Ulaya na duniani. Ottmar yupo kwenye orodha ya makocha wabeba kabisa waliobeba mataji makubwa mengi. Mataji yake 14 aliyobeba Ujerumani alifanya hivyo kwa nyakati zake mbili tofauti alizokuwa kwenye kikosi cha Bayern Munich. Hitzfeld alikwenda kufurahia pia nyakati bora kabisa za kazi yake ya ukocha kwenye kikosi cha Grasshopers ya Uswisi na aliinoa pia Borussia Dortmund ya Ujerumani. Wakitajwa makocha waliokuwa na mafanikio makubwa kwenye soka, Hitzfeld jina lake haliwezi kuwekwa kando hata mara moja.


6. Luiz Felipe Scolari (mataji 26)

Mbrazili, Luiz Felipe Scolari aliwahi kupata kazi ya kuinoa Chelsea baada ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Dunia 2002, ambapo aliwachapa Ujerumani kwenye mchezo wa fainali na kushinda ubingwa kwenye fainali hizo zilizofanyika Japan na Korea Kusini. Kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu nyingi sana, hakufanya jambo la maana Chelsea, lakini alipita Gremio, Palmeiras na Guangzhou Evergrande na kuweka alama zake. Scolari ni miongoni mwa makocha waliobeba mataji mengi makubwa kwenye maisha yao ya soka, akifanya hivyo mara 26 na kuingia kwenye orodha ya makocha wababe kabisa duniani.


5. Jock Stein (mataji 26)

Gwiji la kweli kwenye kikosi cha Celtic. Wakati sasa kikosi hicho cha miamba ya Scotland kikipita kwenye nyakati ngumu, huku nyuma mambo yao yalikuwa bomba kwelikweli na kutamba hasa katika kipindi walichokuwa chini ya Jock Stein. Kocha Stein alidumu na Celtic kwa miaka 13 na ndani ya muda huo, alishinda ubingwa wa ligi mara 10, huku akienda kuwapa ubingwa maarufu zaidi kwenye kikosi chao, waliponyakua Kombe la Ulaya msimu wa 1966/67. Miaka ya karibuni, Celtic imeonekana kupoteza makali yake hasa kwa msimu huu na kushuhudia mahasimu wao Rangers wakitamba na kutikisa.


4. Valeriy Lobanovskyi (mataji 29)

Mtu aliyejitolea kwa dhati kabisa katika mchezo wa soka. Valeriy ni kocha wa muda kidogo kwenye mchezo huo wa soka, lakini mchango wake kwenye soka bado unahesabika kuwa juu na daima atakuwa mwenye kukumbukwa. Kati ya mwaka 1974 na 2001, Lobanovskyi aliongoza Dynamo Kiev kushinda mataji 13 ya ligi, huku pia alinasa mataji mengine kadhaa akiwa na kikosi hicho, ikiwamo makombe lawili ya Kombe la Washindi barani Ulaya. Kwa rekodi hizo, Valeriy ameingia kwenye orodha ya kuwa kocha namba nne aliyebeba mataji mengi makubwa kwenye historia yake ya mchezo wa soka akifanya hivyo mara 29.


3. Pep Guardiola (mataji 30)

Jumapili iliyopita, kocha Mhispaniola Pep Guardiola aliongoza Manchester City kunyakua ubingwa wa Kombe la Ligi, huku kikosi chake hicho ndani ya msimu huu kikiwa kwenye nafasi nzuri ya kunyakua taji la Ligi Kuu England na wametinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kombe la FA walilitema wiki iliyopita baada ya kuchapwa na Chelsea kwenye mchezo wa nusu fainali. Hayo yote yakiwa mafanikio ya timu ya Guardiola kwa msimu huu, kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich ameingia kwenye orodha ya makocha waliobeba mataji mengi makubwa, akifanya hivyo mara 30 hadi sasa.


2. Mircea Lucescu (mataji 34)

Kocha Mircea Lucescu huko nyuma aliwahi kuingoza Shakhtar Donetsk kubeba mataji manane ya Ligi Kuu Ukraine na Jumapili iliyopita alishinda taji lake la 34 kubwa kabisa kwenye maisha yake ya ukocha. Safari hii amefanya hivyo akiwa na kikosi cha Dynamo Kiev na hivyo kuingia kwenye rekodi za kuwa kocha aliyenasa mataji mengi zaidi katika maisha yake ya soka. Kiwango hicho kimemfanya ashike namba mbili kwenye orodha ya makocha walionasa mataji makubwa kwenye maisha yao ya soka.


1. Sir Alex Ferguson (mataji 48)

Kocha bora kabisa katika historia ya mchezo wa soka na hilo halina mjadala. Kocha Alex Ferguson alishinda ubingwa wa Ligi Kuu England mara 13 katika nyakati zake alizokuwa kwenye kikosi cha Manchester United na kuwa kocha aliyebeba taji hilo mara nyingi kuliko yeyote.

Kuna kocha mwingine atakayekuja kuvunja rekodi yake? Hilo ni jambo la kusubiri na kuwapo kwa uvumilivu mkubwa kwa makocha kudumu na timu moja kwa muda mrefu, kwani Ferguson alifanya hivyo baada ya zaidi ya miongoi miwili. Kwa ujumla wake, Ferguson amebeba mataji makubwa mara 48.

Advertisement