Wasaudia wazidi kukomaa kwa Vinicius Jr

Muktasari:
- Inaelezwa kwamba viongozi wa juu wa Ligi Kuu Saudi Arabia (Saudi Pro League) ndio wanapambana kufanya kila liwezekanalo ili atue.
TIMU za Saudi Arabia bado zina mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid na Brazil, Vinicius Jr, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Inaelezwa kwamba viongozi wa juu wa Ligi Kuu Saudi Arabia (Saudi Pro League) ndio wanapambana kufanya kila liwezekanalo ili atue.
Awali iliripotiwa kuwa matajiri hao wa mafuta wapo tayari kutoa zaidi ya Pauni 200 milioni kama ada ya uhamisho ili kukamilisha dili la mchezaji huyo.
Pia iliripotiwa Vinicius mwenyewe hana furaha Real Madrid na anataka kuondoka Hispania hususan baada ya kukosa tuzo ya Ballon D’or aliyokuwa anapewa nafasi kubwa ya kuichukua mwaka jana.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 ambapo msimu huu amecheza mechi 25 za michuano yote na kufunga mabao 14.
Licha ya uwezekano mdogo wa dili hilo kukamilika kutokana na umuhimu wa Vinicius katika kikosi cha Real Madrid, taarifa zinaeleza Waarabu wanataka kutoa ofa ambayo wanaamini itakuwa staa huyo kuikataa. Miongoni mwa timu anazoweza kutua ni Al-Hilal au Al Nassr.
Douglas Luiz
MANCHESTER City inataka kumsajili kwa mkopo kiungo wa Juventus na Brazil, Douglas Luiz, 26, katika dirisha hili la usajili, lakini mchakato unaonekana kuwa mgumu kwani Juventus inataka kuwepo na kipengele kitakachowalazimu kumnunua mazima baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika. Luiz ambaye anahitajika kwa mkataba wa miezi sita, msimu huu amecheza mechi 19 za michuano yote.
Trevoh Chalobah
CHELSEA ipo tayari kumuuza beki raia wa England, Trevoh Chalobah ambaye imemrudisha kutoka Crystal Palace alipokuwa akicheza kwa mkopo. Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun fundi huyo mwenye umri wa miaka 25, anaweza kuuzwa ikiwa timu inayomtaka italipa kiasi kisichopungua Pauni 40 milioni. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2030, ambapo hajaichezea Chelsea kwa muda sasa.
Antony
INAELEZWA Jumapili iliyopita huenda ndio ilikuwa mara ya mwisho kwa winga wa Manchester United na Brazil, Antony kuonekana na jezi ya timu hiyo kwani tayari Mashetani hao Wekundu wameshafanya makubaliano na Real Betis inayomtaka katika dirisha hili. Antony, 24, ni mmoja wa mastaa ambao hawapati nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha Man United.
Jamie Gittens
MANCHESTER United na Chelsea zimeanza mapambano ya sirisiri kuwania saini ya kiungo wa Borussia Dortmund, Jamie Gittens, 20, ambaye pia huduma yake inahitajika na Bayern Munich. Staa huyo wa kimataifa wa England, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2028.Msimu huu tayari amecheza mechi 26 za michuano yote.
Alphonso Davies
REAL Madrid imepanga kuachana na mchakato wa kumsajili beki wa kushoto wa Bayern Munich na Canada, Alphonso Davies, 24, ambaye anadaiwa kubadilisha mawazo yake ya kutaka kuondoka badala yake atabaki na kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye viunga hivyo. Awali Davies aliripotiwa kuwa na nafasi kubwa ya kutua Real Madrid.
Harvey Elliott
BORUSSIA Dortmund imefikia patamu katika mazungumzo na Liverpool kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa timu hiyo na England, Harvey Elliott, 21, katika dirisha hili. Elliot amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Liverpool tangu kuanza kwa msimu huu, jambo linalosababisha ahusishwe kuondoka katika dirisha hili.
Lloyd Kelly
JUVENTUS inataka kumsajili beki kisiki wa Newcastle United, Lloyd Kelly, 26, ambaye ameichezea timu hiyo kwa miezi saba tangu ajiunge akitokea Bournemouth kwa usajili huru majira ya kiangazi mwaka jana. Kelly ambaye ni mmoja kati ya mastaa tegemeo wa Newcastle, anasajiliwa kwa ajili ya kuziba pengo la Andrea Cambiaso anayehusishwa kuondoka.