Wachezaji matajiri wakutana Euro 2024

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kutokana na kuwapo na mishahara mikubwa kwenye mchezo wa soka pamoja na dili za kibiashara za mamilioni, zinafanya masupastaa wa soka kama Cristiano Ronaldo na Kylian Mbappe kuwa na mkwanja mrefu, ambapo hata kama wakiamua kustaafu sasa, hivi wataishi maisha ya raha tu.

MUNICH, UJERUMANI: EURO 2024 imekusanya mastaa wa maana kwenye soka watakaoonyeshana kazi, lakini unamjua ni nani mwenye mkwanja mrefu kuzidi wengine?

Kutokana na kuwapo na mishahara mikubwa kwenye mchezo wa soka pamoja na dili za kibiashara za mamilioni, zinafanya masupastaa wa soka kama Cristiano Ronaldo na Kylian Mbappe kuwa na mkwanja mrefu, ambapo hata kama wakiamua kustaafu sasa, hivi wataishi maisha ya raha tu.

Hata supastaa wa England, Jude Bellingham, ambaye ana umri wa miaka 20, naye mkwanja wake ni mrefu kutokana na dili safi za matangazo.

Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya mastaa wa soka matajiri wanaokipiga kwenye Euro 2024 huko Ujerumani.

1.Cristiano Ronaldo (Pauni 471milioni); Supastaa huyo wa Ureno, Ronaldo, 39, atacheza fainali zake za sita kwenye michuano ya Ulaya, atapangwa Jumanne dhidi ya Czech Republic. Inaaminika hizi zitakuwa fainali zake za mwisho za Ulaya akiitumikia Ureno. Mwaka 2020 aliripotiwa kufikia utajiri wa Dola 1 bilioni na Forbes, inaripoti kwamba aliingiza Pauni 164 milioni kwa dili za ndani ya uwanja. Ronaldo alipiga Pauni 47 milioni kwenye dili za kibiashara, huku pato lake likiripotiwa kufikia Pauni 471 milioni.

2.Kylian Mbappe (Pauni 141milioni); Alianza kuichezea Ufaransa mwaka 2017 na tangu wakati huo Kylian Mbappe amekuwa mchezaji mkubwa kwenye mchezo wa soka duniani. Kipato chake ni Pauni 141 milioni na hilo linamfanya awe mchezaji namba mbili kwa utajiri kwa wakali waliopo kwenye fainali za Euro 2024. Akiwa na umri wa miaka 25 tu, tayari ameshabeba mataji makubwa, ikiwamo Kombe la Dunia 2018.

3.Harry Kane (Pauni 72milioni); Straika, Harry Kane ndiye kinara wa mabao wa muda wote kwenye kikosi cha England. Alishuhudia pato lake likiongezeka kwa Pauni 24 milioni ndani ya mwaka mmoja tu na hivyo kuwa na kipato cha jumla, Pauni 72 milioni. Kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi, ambapo mwaka 2023, alibamba dili tamu huko Bayern Munich linalomshuhudia akilipwa Pauni 21.5 milioni kwa mwaka. Alipotua Allianz Arena, alilipwa Pauni 30 milioni za usajili, huku dili zake za nje ya uwanja zikimwingizia Pauni 13 milioni.

4.Antoine Griezmann (Pauni 71milioni); Supastaa wa Ufaransa, Antoine Griezman, 33, anaripotiwa kuwa na kipato kinachofikia Pauni 71 milioni.

Mshahara mkubwa aliowahi kulipwa wa Pauni 21 milioni kwa mwaka, ulimfanya kuingia kwenye orodha ya wanasoka 10 wanalipwa kibosi kwa miaka ya karibuni. Nje ya uwanja, Griezmann amevuna Pauni 4.7 milioni kwenye dili za matangazo ya kibiashara.

5.Robert Lewandowski (Pauni 67milioni); Ufundi wa ndani wa uwanja wa straika huyo wa Poland, Robert Lewandowski umemfanya staa huyo ashinde tuzo kadhaa za ubora mwaka 2020. Jambo hilo limekwenda sambamba na kudaka dili za maana kabisa, ambapo kwa mwaka huo aliripotiwa kuingiza Pauni 23.5 milioni kwenye mshahara na kuwa mmoja wa wanasoka wanaolipwa kibosi. Pato la Lewandowski ni Pauni 67 milioni.

6.Kevin De Bruyne (Pauni 56milioni); Kevin De Bruyne amekuwa mmoja wa wachezaji wanaoaminika zaidi kwenye kikosi cha Ubelgiji kwa miaka ya karibuni. Kiungo huyo mchezeshaji wa Manchester City anaripotiwa kuwa na pato linalofikia Pauni 56 milioni. Mshahara wa staa huyo kwa mwaka umeripotiwa kuwa Pauni 15.7 milioni na hivyo kuwamo kwenye orodha ya wanasoka matajiri waliopo kwenye Euro 2024 huko Ujerumani.

7.Luka Modric (Pauni 58.9milioni); Mafanikio yake ya ndani ya uwanja yamekwenda sambamba pia na kwenye akaunti yake ya benki. Staa huyo, ambaye atakuwa na kikosi cha Croatia kwenye fainali hizo za Euro 2024, anaripotiwa kuwa na kipato kinachofikia Pauni 58.9 milioni. Mshahara wake wa mwaka kwa huduma anayotoa kwenye timu ya Real Madrid unakadiriwa ni Pauni 7.8 milioni.

8.Romelu Lukaku (Pauni 50milioni); Straika wa Ubelgiji, Romelu Lukaku anaaminika kuwa na kipato kinachofikia Pauni 50 milioni. Staa huyo alipita kwenye timu nyingi kama za Manchester United, Inter Milan na Chelsea na kupiga pesa za kutosha, huku ripoti zikidai mshahara wake wa mwaka ni Pauni 6.3 milioni kwa huduma yake aliyokuwa akitoa huko AS Roma kwa mkopo. Lukaku ni mmoja ya watu wenye pesa huko Euro 2024.

9.Thomas Muller (Pauni 45milioni); Gwiji wa Ujerumani, Thomas Muller, 34, amevuna pato la Pauni 45 milioni katika maisha yake ya soka hadi sasa. Kwenye soka amebeba mataji ya kutosha pia, ikiwamo Bundesliga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Dunia. Kwa mwaka kwa huduma yake anayotoa kwenye kikosi cha Bayern Munich imeripotiwa kuwa Pauni 18 milioni, huku wiki akipokea Pauni 345,000.

10.Jude Bellingham (Pauni 40milioni); Pato la kiungo wa England na Real Madrid, Jude Bellingham linakadiriwa kufikia Pauni 40 milioni hiyo ni baada ya kukamilisha dili lake la uhamisho wa Pauni 103 milioni kutoka Borussia Dortmund kwenda Los Blancos mwaka jana. Mshahara wake wa mwaka unaripotiwa kuwa Pauni 11.6 milioni, huku kwa wiki akiweka kibindoni Pauni 200,000. Ana dili tamu pia za matangazo ya kibiashara zinazomwingizia pesa ya kutosha na hivyo kumfanya Bellingham kuwa miongoni mwa wanasoka matajiri waliopo kwenye Euro 2024.