Vigogo Madrid watia maguu kwa Rodri
Muktasari:
- MABOSI wa Real Madrid wamepanga kumsajili kiungo wa Manchester City na Hispania Rodri, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo mkataba wake utakuwa umebakisha miaka miwili kabla ya kumalizika.
MABOSI wa Real Madrid wamepanga kumsajili kiungo wa Manchester City na Hispania Rodri, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo mkataba wake utakuwa umebakisha miaka miwili kabla ya kumalizika.
Madrid imevutiwa sana na kiwango cha Rodri alichoonyesha msimu uliopita akiwa na Hispania na Man City ambapo alicheza mechi 50 za michuano yote, akafunga mabao tisa na kutoa asisti 14.
Rodri ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Man City lakini msimu huu umeanza vibaya akiwa hajacheza hata mechi moja kutokana na majeraha yanayomwandama.
Licha ya mkataba wake kuwa unamalizika mwaka 2027, hadi sasa bado hajasaini mkataba mpya licha ya ripoti kudai kwamba Man City imemwekea ofa hiyo mezani.
Inaelezwa Rodri amesitisha mpango wa kusaini dili jipya hadi mwisho wa msimu akisubiria kuona kama kocha Pep Guardiola ambaye mkataba wake unamalizika mwakani ataondoka ama atabaki.
GALATASARAY ipo tayari kumchukua kiungo wa Manchester United, Casemiro kwa mkopo na kulipa mshahara wake wa Pauni 300,000 kwa wiki lakini staa huyo wa kimataifa wa Brazil anadaiwa kuwa hataki kuondoka kwa sasa na badala yake anataka kupambania namba kwenye kikosi cha kwanza.
Casemiro ambaye mkataba wake unamalizika mwakani, anahusishwa kuondoka kwa sababu ameanza vibaya msimu huu.
ISTANBUL Basaksehir inadaiwa kuwa tayari kulipa mshahara wote wa beki wa Newcastle United, Kieran Trippier ili kuipata huduma yake kwa mkopo wa msimu mmoja.
Trippier anahusishwa kuondoka tangu kuanza kwa msimu huu kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza na kwa umri wake anachohitaji kwa sasa ni kucheza tu.
BEKI wa Real Madrid na Hispania, Dani Carvajal, ameweka wazi kuwa anatamani kucheza soka nchini Marekani kabla ya kustaafu kucheza mchezo huo.
Carvajal mwenye umri wa miaka 32, mkataba wake na Madrid unatarajiwa kumalizika mwaka 2025. Msimu uliopita alicheza mechi 41 za michuano yote na kutwaa Ligi ya Mabingwa, La Liga na Euro 2024.
MABOSI wa Newcastle bado wanahitaji huduma ya beki wa Crystal Palace na England, Marc Guehi lakini imepanga kurudi tena mezani katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Newcastle iliona kuendelea kufanya mazungumzo na Palace juu ya staa huyo wakati ligi imeshaanza isingekuwa jambo la busara. Mkataba wa Guehi unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
KUNA uwezekano mkubwa Newcastle ikaingia tena katika mazungumzo na Burnley kwa ajili ya kuipata saini ya kipa wa timu hiyo, James Trafford katika dirisha la majira ya baridi mwakani ambapo atakuwa amebakisha mwaka mmoja na nusu katika mkataba.
Taarifa zinadai Newcastle ilitamani sana kumsajili Trafford kwa mkopo katika dirisha la majira ya kiangazi lililopita.
TOTTENHAM imeripotiwa kutaka kutuma ofa kwenda Barcelona Januari mwakani ili kuipaTa saini ya beki wa timu hiyo na Denmark, Andreas Christensen, 28.
Andreas ambaye msimu uliopita alicheza mechi 42 za michuano yote, inaonekana kuwa tayari kumwachia kutokana na hali yao ya kiuchumi.
Nyota kadhaa wanaruhusiwa kuondoka ili kubalansi vitabu vya hesabu.
ATLETICO Madrid imepanga kurudi tena mezani katika mazungumzo na mabosi wa Manchester City katika dirisha lijalo la majira ya baridi ili kuipata huduma kiungo wa timu hiyo na Ureno, Matheus Nunes kwa mkopo wa nusu msimu.
Nunes anadaiwa kuhitaji kuondoka Man City kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.