Uholanzi yawakuta Ujerumani
Muktasari:
- Maofisa wa Uholanzi walilazimika kutafuta usafiri mbadala na kwa muda huo walichukua basi ambalo liliongozwa na king’ora cha polisi ikiwa ni sehemu ya usalama kurudi hotelini.
DORTMUND, UJERUMANI: KABLA ya kukutana na England katika Uwanja wa Signal Iduna Park, Uholanzi ilipata shida ya usafiri baada ya kukwama kwa muda katika kituo cha treni kabla ya kuibuka kwa taarifa huduma ya treni kutoka Wolfsburg kwenda Dortmund zimesitishwa.
Maofisa wa Uholanzi walilazimika kutafuta usafiri mbadala na kwa muda huo walichukua basi ambalo liliongozwa na king’ora cha polisi ikiwa ni sehemu ya usalama kurudi hotelini.
Uholanzi ilikuwa inatakiwa ifike Dortmund kabla ya saa 1:45, usiku Jumanne kwa saa za Ujerumani kwa ajili ya mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi lakini ilishindikana na ikakodi ndege ya kuondoka saa 2:20 usiku kwa saa za Ujerumani.
Hiyo ilisababisha wakose kutembelea uwanja siku moja kabla ya mchezo kama inavyofanywa na timu nyingi kwani badala ya kufika Jumanne alasiri, waliingia Dortmund saa tisa usiku wakiwa wamesafiri maili 200 kwa ndege.
Viwango vya joto, Ujerumani vilipanda hadi kufikia nyuzi joto 33 Jumanne, ingawa kinatarajiwa kushuka katika mchezo huo wa saa nne usiku wa kuamkia leo.
Uefa imezitaka timu zote kuhakikisha zinaepuka usafiri wa ndege kadri iwezekanavyo kwani wanahitaji kufanya mashindano hayo kuwa rafiki na moja ya njia za kufanikisha hilo ni timu kupanda treni na huwa wanachangamana sana na watu hata wale wa hali za chini.
Baada ya kuchelewa kufika katika muda uliopangwa, mkutano uliahirishwa na badala yake makocha wakahojiwa kwa njia ya video mtandao (Zoom).
Usafiri wa treni Ujerumani unadaiwa kusumbua sana na mashabiki wamekuwa wakikumbana na matatizo ya kuchelewa na kuahirishwa safari mbalimbali.