UEFA utamu kolea, mambo ni moto balaa

BARCELONA, HISPANIA. ULE utamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya umerudi tena na leo Jumanne na kesho Jumatano kuna mechi zinapigwa kabla ya kumalizana tena wiki ijayo kusaka timu zitakazofuzu hatua ya 16 bora.

Nani atapita? Ni swali lililopo kwa sasa. Hata hivyo kuna timu ambazo zimeshajihakikishia kufuzu na ambazo zinahaha kupata matokeo ili zifuzu hatua hiyo.

Kati ya timu ambazo zinauhakika wa kufuzu ni Bayern Munich na katika kundi lake E miamba hiyo ina alama 12 kabla ya mchezo wa leo huku wenzake kwenye kundi hilo, Barcelona, ina sita, Benfika nne na Dynamo Kyiv ina moja.

Bayern itakuwa ugenini kuanzia saa 2:45 usiku kumenyana na Dynamo Kiev huku Barcelona chini ya kocha mpya Xavi Hernandez itakuwa nyumbani kuikaribisha Benfika kupambania nafasi mbili za juu ili kufuzu.

Mechi ambayo inatarajiwa kuteka hisia za wengi ni ile ya Manchester United dhidi ya Villarreal, kibarua kikiwa kikubwa kwa Man United iliyotoka kumfukuza kazi kocha wake, Ole Gunnar Solskjaer na Michael Carrick na Darren Fletcher wataongoza jeshi hilo linaloongoza msimamo wa kundi lao kwa alama saba sawa na wapinzani wao Villarreal huku Atalanta na Young Boys zikiwana na alama tano na tatu mtawalia. Man United inahitaji kushinda mchezo huo na ujao wiki ijayo ili kuweka hai matumaini ya kufuzu hatua hiyo.

Kundi H linaloongozwa na Juventus yenye alama 12 presha ipo pale Stamford Bridge, London leo miamba hiyo itakapomenyana kusaka nafasi ya kwanza. Chelsea yenye alama tisa inahitaji ushindi dhidi ya vinara hao ili kumaliza kileleni hukiu Zenit na Malmo zikiwa na matumaini finyu kutokana na matokeo mabovu waliyoyapata na zenyewe zitamalizana kuanzia saa 5:00 usiku.

Hivyo Chelsea itatakiwa kushinda mechi mbili za mwisho ili kufikisha pointi 13 huku ikiombea mabaya Juve kwenye mechi zake zote mbili ikiwamo dhidi yao leo usiku saa 5:00.

Kundi G leo litazikutanisha Lille yenye alama tano ikiwa nafasi ya pili dhidi ya vinara wa kundi hilo Salzburg yenye alama saba. Sevilla wenyewe wataikaribisha Wolfsburg na kwenye kundi hilo lolote linaweza kutokea kulingana na matokeo ya michezo miwili iliyobaki kukamilisha hatua ya makundi.

Kesho Jumatano kutakuwa na kibarua kingine na kundi A kutakuwa na kibarua kigumu kwa Manchester City itaikaribisha PSG kuanzia saa 5:00 zikiwania kumaliza kileleni mwa kundi hilo ambalo kwa sasa vinara ni Man City ikiongoza kwa alama tisa ikifuatiwa na PSG yenye alama nane huku Club Brugge ikiwa na nne na RB Leipzig ikiburuza mkia na alama moja.

Kazi ipo kwa City, PSG na Club Brugge ambazo kwa michezo miwili iliyosalia zinawania nafasi ya kwanza na ya pili ili zifuzu. Lolote linaweza kutokea. Kundi B vinara wake ni Liverpool ikiwa na alama 12 ikifuatiwa na FC Porto yenye tano, huku Atletico Madrid ikiwa na nne na AC Milan moja.

Shughuli pevu itakuwa kwa FC Porto na Atletico kuwania nafasi ya pili kwani vinara Liverpool tayari wameshajihakikishia nafasi ya kufuzu ikichangiwa na moto wao msimu huu.

Kundi C vinara Ajax iliyo moto msimu huu tayari imefuzu kutokana na kuwa na alama 12 huku inayofuatia Borrusia Dortmund ikiwa na sita sawa na Sporting CP huku Besiktas ikipuruza mkia bila alama.