Ten Hag: Tuliwapiga, wapigeni tena

MANCHESTER, ENGLAND. ERIK ten Hag amewaambia wachezaji wake “tuliwapiga mara moja, wapigeni tena” wakati alipokuwa akiwaandaa na mchezo dhidi ya Arsenal.

Manchester United ni timu pekee iliyoichapa Arsenal kwenye Ligi Kuu England msimu huu wakati walipowashushia kipigo cha mabao 3-1 uwanjani Old Trafford, Septemba 4, mwaka jana.

Na tangu wakati huo, Arsenal ya Mikel Arteta imeshinda mechi 10 na kutoka sare mbili na sasa wapo kileleni kwenye msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano na wana mechi moja mkononi. Lakini, mchezo wa leo Jumapili ni mgumu, kwani Arsenal itaingia uwanjani huko Emirates baada ya mechi ya Manchester City na Wolves huko Etihad, ambayo hadi muda huo pengo la pointi linaweza kuwa mbili kama Pep Guardiola atashinda.

Kocha Ten Hag alisema: “Wapo vizuri. Wana ari fulani kwenye timu, lakini sisi tunajua cha kufanya. Ni juu yetu kuwapiga na tutafanya kila tunaloweza kutimiza hilo. Yatupasa tuwe vizuri. Tunahitaji kiwango kizuri. Kama tutafanya hivyo, ninaamini nitakuwa na nafasi nzuri ya kwenda kupata matokeo.”

Ten Hag alipuuza wasiwasi kukosekana kwa Casemiro, ambapo kiungo huyo alionyeshwa kadi ya njano ya tano kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Crystal Palace, Jumatano iliyopita.

Ten Hag alisema: “Tuliwapiga Arsenal mara ya mwisho bila ya Casemiro. Tunayo njia sahihi ya kukabiliana na vitu kama hivyo.”Ten Hag aligoma kufichua Jadon Sancho atarejea lini mzigoni.