Ten Hag awekewa mtego United

MANCHESTER ENGLAND. MIFUKO ya Erik ten Hag itajazwa mkwanja mrefu baada ya mabosi wa Manchester United kumwambia kwamba watampa bonasi ya Pauni 3 milioni endapo atairudisha timu hiyo kwenye Ligi Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kuboronga msimu uliopita.

Ten Hag anavuta mshahara wa Pauni 9 milioni kwa mwaka, nusu ya mshahara anaopewa Pep Guardiola kule Manchester City na tayari Mholanzi huyo ana kibarua kizito kuhakikisha Man United inafanya vizuri msimu mpya utakapoanza.

Endapo Man United itashindwa kutinga katika michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya, mara mbili mfululizo itapata hasara ya Pauni 90 milioni, jambo ambalo linawapasua vichwa mabosi wa klabu hiyo.

Vilevile Man United itapata hasara nyigine ya Pauni 25 milioni, ambayo itakatwa kutoka katika kampuni ya Adidas kama kipengele cha makubalino yao, endapo itashindwa kufuzu Ligi Mabingwa Ulaya msimu ujao. Adidas imeidhamini Man United kwa Pauni 75 milioni kwa mkataba wa miaka 10.

Man United pia itapoteza pesa kwa wadhamini wao wa jezi Team Viewer, kwani wameweka bonasi ya Pauni 47 milioni endapo vijana wa Ten Hag watafanikiwa msimu huu.

Kwa mujibu wa ripoti, Man United itapoteza pesa nyingi msimu huu ikiboronga, kupitia kampuni kadhaa kubwa ambazo zimeweka pesa kuidhamini klabu hiyo iliyopoteza mvuto katika miaka ya hivi karibuni.

Wakati huohuo, Man United imeendelea kujiimarisha kwenye mechi za maandalizi ya msimu mpya, hata hivyo juzi ilitoka sare ya mabao 2-2, ilipomenyana na Aston Villa, baada ya kushinda mfululizo mechi tatu za awali za kirafiki.