Spurs yaachana na Mourinho

LONDON, ENGLAND. TOTTENHAM imeachana na kocha wake Jose Mourinho ikiwa ni miezi 17 tangu aanze kazi ya kuinoa timu hiyo.
Spurs imeachana na Mourinho kutokana na muenendo mbaya wa timu hiyo kwa msimu huu ambapo ipo katika nafasi za chini kwenye Ligi Ku na haina matumaini ya kushiriki michuano ya  Europa League kwa msimu ujao.
Mourinho, 58, alikuwa kwenye presha kubwa kutokana na matokeo ya timu hiyo kwenye siku za hivi karibuni na hatimaye bosi wa Spurs, Daniel Levy akaamua kuvunja mkataba wake ikiwa ni siku sita kabla ya mchezo wao wa fainali ya Carabao dhidi ya Manchester City.
Fundi huyo kutoka Ureno alichukua mikoba Novemba 2019, baada ya Mauricio Pochettino kufungashiwa virago na alisaini mkataba ambao ungemalizika msimu wa 2022-23.
Kiungo wa zamani wa timu hiyo Ryan Mason ndio anatarajiwa kuchukua mikoba akisaidiana na  Chris Powell hadi mwisho wa msimu.
Inaaminika kuwa tayari mchakato wa kumtafuta mrithi wa Mourinho umekwishaanza na atatangazwa katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi huku taarifa za ndani zikidai kwamba ni kocha wa RB Leipzig, Julian Nagelsmann.
Mourinho ameiacha Spurs ikiwa nafasi ya saba kwa alama 50 ilizokusanya kwenye mechi 32 na mchezo wa mwisho alitoa sare na Everton.