Sancho? subirini mtamuona

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Erik ten Hag amesema winga wake Jadon Sancho atakinukisha tu, baada ya kucheza kwa mara ya kwanza akitokea benchi kwenye mechi pili ya nusu fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Nottingham Forest.
Ten Hag amemsifia winga wake kwa mapokezi mazuri aliyopata uwanja wa Old Trafford akisisitiza anaamini atakuwa ana mchango mkubwa kwenye timu baada ya kurudi kikosini.
Mashabiki wa Man United walimpigia makofi Sancho alipoingia uwanjani akitokea benchi jambo ambalo lilimfurahisha Mholanzi huyo, ikumbukwe winga huyo wa kimataifa wa England alikuwa nje ya dimba tangu Oktoba mwaka jana, ilielezwa Sancho alikuwa akisumbuliwa na matatizo binafsi iliyopelekea kiwango chake kushuka lakini sasa amerejea kukiwasha.
Akizungumza baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nottingham kwenye mechi ya nusu fainali ya pili ya Kombe la Carabao, Ten Hag alisema wachezaji wenye vipaji kama Sancho wanastahili kufurahia soka kwasababu ndio kazi inayowalipa.
"Ni jambo zuri mashabiki wamemkaribisha kwa shangwe, nadhani itamsaidia katika safari yake ya mapambano, ndio kwanza ameanza, alifanya mazoezi kwa bidii kwa muda wa wiki mbili, tumeona tabasamu na tunamuombea aendelee na ari hiyo," alisema Ten Hag
Man United ilitinga fainali ya Kombe la Carabao kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa Nottingham jumla ya mabao 5-0, katika fainali yao ya kwanza mashetani wekundu waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mabao ya Man United yaliwekwa kimiani na Anthony Martial aliyefunga dakika ya 73, Fred akacheka na vyavu dakika ya 76 ya mtanange huo. Martial alirejea pia baada ya kupona majeraha.
Man United itacheza fainali ya Kombe la Carbao Cup kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017 na itamenyana dhidi ya Newcastle kwenye mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Wembley Februari 26 mwaka huu.