Richarlison atoboa siri ya Conte

LONDON, ENGLAND. STRAIKA wa Tottenham, Richarlison ameweka wazi kwamba Antonio Conte ndiye aliyemshawishi kujiunga na timu hiyo katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwezi uliopita akitokea Everton.

Richarlison alivunja rekodi ya usajili Spurs ilipomsajili kwa kitita cha Pauni 60 milioni akasaini mkataba mrefu utakaodumu hadi mwaka 2027.

Staa huyo wa kimataifa Brazil amesifiwa na mashabiki baada ya kufunga mabao mawili na kutoa asisti katika mechi nane alizocheza mashindano yote msimu huu.

Richarlison amesema Chelsea ilimpa ofa kabla ya Conte kuingilia kati dili hilo kwa kumpigia simu ya mkononi na kumshawishi ajiunge na Spurs msimu huu.

“Chelsea ilinipa ofa pamoja na Arsenal, timu hizi ziliwasiliana na Everton ili kujua kuhusu msimamo wangu, lakini Tottenha, ikaingilia kati na kutoa pesa zote, nilikuwa mapumziko nyumbani (Brazil) niliposikia Spurts imewasiliana na Everton kwaajili yangu, nilifurahi sana niliposikia taarifa hiyo, Conte alinipigia simu kwenye makubaliano hayo na kunishawishi pia,” alisema.

Richarlison alikuwa nyota wa mchezo kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Ghana wikiendi iliyopita alipoifungia Brazil mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0.

Straika huyo anatarajiwa kuwepo katika mechi ijayo ya Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal, mtanange unaotabiriwa kuwa mkali kutokana na ubora wa timu hizi msimu huu.

Conte anaamini ataitibulia Arsenal iliyoanza msimu kwa kishindo licha ya kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Man United.