Rasmi Bayern Munich yatua kwa Kobbie Mainoo

Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti, Mainoo amekataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Man United kutokana ofa ndogo iliyowekwa na mabosi wa timu hiyo.
BAYERN Munich imeingia kwenye vita dhidi ya Chelsea kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa Manchester United na England, Kobbie Mainoo.
Kwa mujibu wa ripoti, Mainoo amekataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Man United kutokana ofa ndogo iliyowekwa na mabosi wa timu hiyo.
Mainoo ambaye kwa sasa anapokea mshahara wa Pauni 20,000 kwa wiki amewaambia vigogo wa Man United na ili asaini mkataba mpya anataka kupewa ofa ya mshahara unaofikia Pauni 200,000 kwa wiki.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, lakini Man United huenda ikamuuza kabla ya mkataba huo kumalizika ikiwa ataendelea kugoma kusaini.
Ripoti zinaeleza timu zinazomhitaji kuwa zipo tayari kumsajili na kumpa ofa ya mshahara unaozidia hiyo Pauni 200,000.
Alejandro Garnacho
Manchester United inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 42 milioni ili kumuuza winga wao raia wa Argentina, Alejandro Garnacho, 20, katika dirisha hiki la majira ya baridi. Hivi karibuni fundi huyu amekuwa akiwindwa sana na Napoli ya Antonio Conte ambaye ndiye amependekeza asajiliwe katika dirisha hili. Msimu huu Garnacho hajawa na kiwango bora na mara kadhaa amekuwa akianzia benchi ingawa kuna kila dalili akasalia United.
Kyle Walker
MANCHESTER City imepanga kumwachia bure beki wao raia wa England, Kyle Walker, 34, dirisha hili. Ripoti zinaeleza huduma ya staa huyu inahitajika na Milan ambayo imeonyesha nia baada ya kocha Pep Guardiola kuweka wazi Walker ameomba kuondoka. Mabosi wa Man City wanataka kumwacha bila ya kuchukua chochote ili kuonyesha heshima kwa mchango wake alioutoa kwa miaka isiyopungua nane akiwa na timu hiyo.
Marcus Rashford
AC Milan imeanza mazungumzo na wawakilishi wa Manchester United kuipata saini ya mshambuliaji wa timu hiyo, Marcus Rashford, 27, dirisha hili. Rashford amekuwa nje ya kikosi cha Man United kwa zaidi ya mechi tatu baada ya Kocha Ruben Amorim kumwondoa akisema haridhishwi na utendaji kazi wake. Mbali ya Milan, saini yake pia inawindwa sana na PSG, Borussia Dortmund na Arsenal.
Donyell Malen
ASTON Villa imekubali kutoa Pauni 19 milioni kwenda Borussia Dortmund kuipata saini ya mshambuliaji wao, Donyell Malen, 25, katika dirisha hili. Donyell ni miongoni mwa mapendekezo ya kocha Unai Emery ambaye anaamini staa huyo ataenda kuboresha eneo lao la ushambuliaji. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Msimu huu amecheza mechi 25 za michuano yote na kufunga mabao sita.
Loic Bade
BEKI kisiki wa Sevilla na Ufaransa, Loic Bade ameingia kwenye rada za Aston Villa ambayo inayohitaji saini yake katika dirisha hili. Loic mwenye umri wa miaka 24,msimu huu amecheza mechi 16 za michuano yote na kutoa asisti moja. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Villa inataka kuimarisha kikosi chake na inapambana kumaliza nafasi za juu kwenye msimamo.
Carney Chukwuemeka
CHELSEA ipo tayari kumwachia kiungo wao, Carney Chukwuemeka, 21, kwa mkopo dirisha hili lakini changamoto imekuwa kwa Carney ambaye bado hajafanya uamuzi wa wapi aende kukiwa na idadi ya timu zinazomhitaji dirisha hili. Miongoni mwa timu zinazohitaji saini yake ni Borussia Dortmund na Strasbourg.
Tyrell Malacia
BEKI wa Manchester United, Tyrell Malacia, 25, huenda akaondoka katika timu hiyo dirisha hili kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza mara kwa mara. Ripoti zinaeleza, Malacia atatolewa kwa mkopo na baadhi ya timu za ndani na nje ya England tayari zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili. Mkataba wake unamalizika mwaka 2026.