Qatar chalii sherehe za ufunguzi zikifana

DOHA,QATAR. MWENYEJI wa fainali za Kombe la Dunia, Qatar imepokea kichapo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa ufunguzi uliochezwa katika uwanja wa Al Bayt jana.
Mabao ya Ecuador yaliwekwa kimiani na Enner Valencia dakika ya 16, bao lingine akipachika kwa mkwaju wa penalti dakika ya 32 baada ya bao lake lingine kukataliwa na mwamuzi kwa kuwa ameotea eneo la hatari.

Aidha staa huyo aliyewahi kukipiga Everton na West Ham alilazimika kutolewa nje ya uwanja baada ya kupata majeraha, mchezo huo ulipokuwa ukiendelea.


Qatar ilistahili kipigo hicho kwani wachezaji wa timu hiyo walicheza kwa kiwango kibovu dakika zote za mtanange huo uliyohudhuriwa na viongozi wengi akiwemo Rais wa Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA), Gianni Infatino.
Kabla ya mtangane huo kulikuwa na burudani mbambali za sherehe za kukaribisha fainali hizi zinazofanyika kwa mara ya kwanza ndani ya falme za kiarabu.
Sherehe zilipambwa na makundi tofauti, mwanamuziki kutoka Korea Kusini, Junkook alitembuiza 'Live' nyimbo yake maalumu ya Kombe la Dunia inaitwa 'Dreamer'.
Mbali na burudani hizo za muziki kulikuwa na tamasha jingine ambalo limeteka hisia za  mashabiki, tamasha hilo limeongozwa na mwigizaji mkongwe wa filamu kutoka Marekani, Morga Freeman.