Palmer, Foden watibua hesabu Uingereza

Muktasari:

  • Kikosi hicho cha England maarufu kama Three Lions kitashuka uwanjani kukipiga na Jamhuri ya Ireland, Jumamosi huko Dublin, kabla ya kukabiliana na Finland, Jumanne ijayo, mechi ambazo zitamshuhudia kocha wa mpito, Lee Carsley akiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza tangu Gareth Southgate alipomwaga manyanga.

LONDON, ENGLAND:COLE Palmer, Ollie Watkins na Phil Foden wamejiengua kwenye kikosi cha England kinachojiandaa na mchezo wa Uefa Nations League kutokana na matatizo tofauti.

Kikosi hicho cha England maarufu kama Three Lions kitashuka uwanjani kukipiga na Jamhuri ya Ireland, Jumamosi huko Dublin, kabla ya kukabiliana na Finland, Jumanne ijayo, mechi ambazo zitamshuhudia kocha wa mpito, Lee Carsley akiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza tangu Gareth Southgate alipomwaga manyanga.

Baada ya ufunguzi wa kiafya waliofanyiwa wachezaji hao kwenye kambi yao huko St. George’s Park, juzi Jumanne, Palmer na Watkins waliruhusiwa kuondoka kwenda kujiunga na klabu zao kwa ajili ya matibabu zaidi.

Staa wa Manchester City, Foden hakuripoti kabisa kwenye kambi ya England baada ya kocha wa miamba hiyo ya Etihad, Pep Guardiola kueleza kwamba winga huyo anasumbuliwa na matatizo ya tumbo na imani kwamba atakuwa fiti baada ya mechi za kimataifa kupita.

Na jambo hilo limemtibulia zaidi mipango ya kocha Carsley, ambaye alihitaji kuwa na mastaa wake wote matata kwenye kikosi ili kusaka matokeo yake bora uwanjani.

Michuano hiyo ya Nations League kwa England inaongozwa na kocha wa muda Carsley, ambaye awali alikuwa kocha wa timu ya England ya U21. Kukosekana kwa Foden, Watkins na Palmer pigo kubwa kwa timu hiyo, iliyofika fainali kwenye fainali za Euro 2024.

Mastaa hao wanaaminika kwamba wanaweza kuwa fiti wakati Ligi Kuu England itakaporejea, Septemba 14. Na wachezaji, kama Noni Madueke, Tino Livramento, Angel Gomes na Morgan Gibbs-White wameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha England.