Pagumu hapo! Liverpool, Man City, Chelsea zina mechi tano za ubingwa

Friday December 31 2021
EPL PIC

LONDON ENGLAND.  GARI la ubingwa wa Ligi Kuu nchini England kwa msimu huu tayari limeshazishusha timu nyingi na timu zinazoonekana kuwa na nauli ya kuendelea na safari ni tatu tu.

Timu ya kwanza ikiwa ni vinara Manchester City yenye alama 50 baada ya kucheza mechi 20, kisha inayofuata ni Chelsea inayoshika nafasi yapili kwa alama 42 baada ya mechi 20 na mwisho ni Chelsea inayoshikilia nafasi ya tatu kwa alama 41 baada ya mechi 20 pia.

Ramani ya ubingwa tayari imeshaanza kuchorwa na Mwanaspoti imezingalia mechi tano zijazo ambazo timu hizi zinatarajia kucheza na mechi hizo zinaweza kuamua nani awe na asilimia 70 au 80 za kuchukua ubingwa msimu huu kwa sababu ni ngumu na zitakuwa zinatoa pointi nyingi.

Ukianzia kwa Manchester City vijana hawa wa Guardiola wanaonekana kwenda kufikia rekodi yao yenyewe ya kushinda mechi 18 mfululizo za Ligi Kuu England ambayo iliwahi pia kuwekwa na Liverpool.

Man City ambayo imefanya vizuri sana kwenye mechi tatu zilizopita ambapo imefunga jumla ya mabao 17, mchezo wake ujao kwenye muendelezo wa Ligi Kuu itacheza dhidi ya Arsenal .

Mechi hii inaweza ikawaathiri kwa sababu Arsenal katika siku za hivi karibuni imeonekana kuimarika sana na imekuwa ikitembeza dozi za kutosha.

Advertisement

Baada ya mechi hiyo wababe hawa watakuwa na mechi ya FA Cup dhidi ya Swindon Town kisha itarudi tena kuichora ramani ya ubingwa kwenye mechi dhidi ya Chelsea, Januari 15 pale Etihad. Mechi hii pia ni ngumu kwa sababu zitakuwa zinakutana timu mbili zinazopambana kuchukua ubingwa msimu huu.

Lakini itakuwa na mechi mbili kwenye hizo tano ambapo moja ndio inatarajiwa kuwa ngumu pale zitakapokutana na Southampton ambayo imefufuka na haijapoteza mechi tatu mfululizo, ikiifunga West Ham na kutoka sare na Tottenham. Mechi ya nne itacheza dhidi ya Norwich inayoonekana kuwa na asilimia nyingi za kushuka daraja hivyo inaweza kujinyakulia alama hapo lakini balaa watakuwa nalo kwa Brentford ambayo mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliwahi kulinda ushindi wa bao 1-0 ili kupata alama tatu.

Alama 15 za mechi tano za Liverpool kwenye EPL zitaanza kutafutwa Januari 02 katika Dimba la Stamford Bridge kwenye mchezo dhidi ya Chelsea, mechi ambayo inatazamiwa kuwa ngumu zaidi kwa sababu timu zote zinajenga orodha ya timu tatu zinazopewa nafasi kubwa zaidi ya kuchukua ubingwa msimu huu.

Baada ya mechi hiyo ya ugenini mchezo mwingine wa ligi utakaowakabili utakuwa dhidi ya Brentford ambayo haitokuwa rahisi kupata pointi kutokana na kiwango chao kwa msimu huu. Vilevile, Liverpool itakuwa na mechi tatu nyingine za kuweka matumaini yao ya ubingwa, mechi ya kwanza ikiwa dhidi ya Crystal Palace ugenini kisha nyumbani dhidi ya Leicester, Burnley zote nyumbani. Mambo hayaonekani kuwa mzuri sana kwa vijana hawa wa Londona katika siku za hivi karibuni kwani imeshinda mechi tatu tu kati ya mechi zao sita za mwisho na wanaonekana kuondoka taratibu kwenye mbio za ubingwa.

Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopita dhidi ya Brighton, Chelsea ambayo inakumbana na shida ya wachezaji wake wasiopungua sita kuambukizwa Corona, watakuwa na mechi dhidi ya Liverpool kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Januari 15, Chelsea itakuwa inaikaribisha Man City kwenye mechi ambayo itawahitaji kushinda ili kuendelea kuweka matumaini ya ubingwa.

Baada ya mechi hiyo watakuwa na kazi ya kuzitafuta alama tatu dhidi ya Tottenham, kabla ya kucheza na Crystal Palace na baadae Leicester City.

Advertisement