Nsue ajiuzulu Equatorial Guinea

Muktasari:

Nsue alimaliza kama mfungaji bora wa Afcon 2023 akiwa na mabao matano

Malabo, Equatorial Guinea - Mshindi wa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, Emilio Nsue, amejiuzulu kuitumikia timu ya taifa ya Equatorial Guinea.


Teodoro Nguema Mangue, makamu wa rais wa nchi hiyo, alithibitisha kustaafu kwa Nsue Jumanne usiku, Februari 20.


Mangue aliandika katika ukurasa wake rasmi wa X (zamani Twitter): "Baada ya majadiliano, nahodha Emilio Nsue Lopez ameamua kujiuzulu kuitumikia timu ya taifa. "Natambua mchango wake wa zaidi ya miaka 12 aliyoitumikia Nzalang Nacional na namtakia mafanikio katika maisha yake ya baadaye."


KUFUNGIWA KWA NSUE

Baada ya fainali za AFCON 2023 zilizofanyika nchini Ivory Coast, Nsue alisimamishwa kwa muda usiojulikana na Shirikisho la Soka la Equatoguinean. Shirikisho hilo lilimtuhumu "kuhusika na matukio mengi utovu wa nidhamu". Katika kujibu tuhuma hizo alitumia akaunti yake ya Instagram kuongea mubashara, akiwa sambamba na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Iban Salvador, ambapo aliwataja vigogo kadhaa wa michezo kama "wanyonya damu, saratani ya soka na wala rushwa."


Salvador pia amefungiwa na Shirikisho la Soka hilo.


Nsue, gwiji wa Equatorial Guinea ambaye ameifungia nchi yake mabao 22 katika mechi 43 za timu ya taifa, ameondoka akiwa ndiye mfungaji kinara wa muda wote wa Equatorial Guinea, akionyesha ubora wake katika soka la ngazi ya juu zaidi Afrika licha ya kuzungukwa na utata katika michuano yake ya mwisho kucheza. Kiraka Nsue bado anaendelea kucheza soka la ngazi ya klabu. Anaitumikia klabu ya Daraja la Tatu Hispania ya Intercity.