Ni robo fainali za rekodi huko Qatar

Muktasari:

  • Fainali za Kombe la Dunia 2022 zinaingia hatua ya ikitarajiwa kuanza kesho ambapo kutakuwa na jumla ya michezo miwili itakayopigwa saa 12:00 jioni na nyingine saa 4:00 usiku.

DOHA, QATAR. HATUA ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia inatarajiwa kuanza kesho ambapo kutakuwa na jumla ya michezo miwili itakayopigwa saa 12:00 jioni na nyingine saa 4:00 usiku.
Mechi ya kwanza itakuwa kati ya Brazil dhidi ya Croatia,  itapigwa pale kwenye dimba la Education  City, maeneo ya Al Rayyan, ndio itakuwa mechi ya mapema kwa kesho na mwamuzi atakayekuwa amesimama kati kati ya  mastaa hao wanaotazamia kuandika historia ni Michale Oliver kutoka nchini England.
Huu unakuwa ni mchezo wa tano kukutanisha mataifa haya kwenye michuano mbali mbali na ni mara tatu kukutana kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Katika mara zote hizo ilizokutana kwenye Kombe la Dunia ilikuwa ni katika hatua za makundi na Brazil ilishinda mechi zote kuanzia ile ya mwaka 2006 ambapo  ilishinda 1-0 na mwaka 2014 ikashinda mabao 3-1.
Mechi nyingine ni za kirafiki ambapo moja iliyochezwa Agosti 2005 ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na mechi nyingine iliyopigwa mwaka 2018 Brazil ilishinda mabao 2-0.
Hivyo kiujumla katika mara zote ambazo timu hizi zimekutana Croatia haijawahi kuonja ladha ya ushindi zaidi imeambulia sare moja na kufungwa mara tatu.
Mechi yapili kwa leo, itapigwa saa 4:00 usiku pale kwenye uwanja utakaotumiwa kuchezea fainali za michuano hii Lusail Iconic Studium, mwamuzi atakayesimama kati kati ni Mhispania Antonio Mateu Lahoz.
Wababe hawa wamekutana mara tisa kwenye michuano mbali mbali  na mara zote hizo Lionel Messi na Argentina yake wamefanikiwa kushinda mara tatu tu, huku Uholanzi ikishinda mara nne na mechi tatu zilizobakia zilimalizika kwa sare.
Katika mechi hizo tisa, tano zimekutana kwenye michuano ya Kombe la Dunia ambapo mara moja ni kwenye fainali, mara mbili hatua ya makundi na mechi mbili zilizobaki ni nusu na robo fainali.
Mara ya kwanza kukutana kwenye Kombe la Dunia  ilikuwa mwaka 1974 kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Uholanzi ikashinda mabao 4-0, ikiwa ni mwezi mmoja tangu zikutane kwenye mechi ya kirafiki ambapo 
Uholanzi iliibuka  na ushindi wa mabao 4-1.
Mwaka 1978 zilikutana kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia kwenye michuano ya mwaka huo iliyofanyika nchini Argentina na mechi imalizika kwa Argentina kushinda mabao 3-1.
Mara ya mwisho kukutana ilikuwa mwaka 2014 kwenye Kombe la Dunia kule nchini Brazil katika nusu fainali na Argentina  imebakiwa na kumbu kumbu nzuri ya kuibuka kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.