Neymar akaribia rekodi ya Pele, Messi noma

RIO, BRAZIL. NYOTA wa timu ya taifa Brazil Neymar Jr, anakaribia kuvunja rekodi ya mkongwe Pele baada ya kufunga bao dhidi ya Tunisia kwenye mechi ya kirafiki uliochezwa usiku wa kuamkia leo.
Neymar alifikisha mabao 75 katika mechi 120 alizoichezea Brazil baada ya kufunga kwa mkwaju wa penalti, akimkaribia Pele aliyefunga mabao 77 anayeshikilia rekodi ya mfungaja bora wa muda wote wa timu ya taifa Brazil.
Mbali na rekodi hiyo Brazil iliichapa Tunisia mabao 5-1, mabao hayo yaliwekwa kimiani na Raphinha dakika ya 11 na 40, Richarlison dakika ya 19 pamoja na Pedro akifunga dakika 74, bao la Tunisia lilipachikwa na Montassar Talbi dakika ya 18.
Neymar anayekipiga Paris Saint-Germain alianza kung'ara kwenye kikosi cha Brazil tangu mwaka 2010 alipokuwa na umri wa miaka 18.
Wakati huohuo Lionel Messi amefikisha mabao 100 katika ngazi ya Kimataifa baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Jamaica kwenye mechi ya kirafiki uliyochezwa usiku wa kuamkia leo Argentina ikitoka na ushindi wa mabao 3-0. Mkali huyo anayekipiga PSG pamoja na Neymar ameanza kwa kishindo msimu huu baada ya kusuasua msimu uliopita alipojiunga akitokea Barcelona.