Messi afungiwa, Barcelona yakata rufaa

Baada ya kupata kadi nyekundu ya kwanza kwenye maisha yake ya soka ndani ya Barcelona staa Lionel Messi (33) amekumbana na rungu la kufungiwa mechi mbili.

Uamuzi huo umetolewa na Shirikisho ka Soka Hispania (RFEF) baada ya Messi aliyekuwa akicheza mchezo wake wa 753 akiwa na jezi ya Barca alimpiga ngumi kichwani Asier Villalibre wa Athletic Bilbao kwenye dakika za lala salama za nyongeza wakati wa mechi ya fainali ya Spanish Super Cup.

Tukio hilo lilibainika kwenye marejeo ya video (VAR) na alionyeshwa kadi nyekundu papo hapo.

Kwa mujibu wa kanuni ya matukio kama hayo yanayotafsiriwa kama ya ugomvi Messi ilibidi afungiwe mechi nne hadi 12 ila RFEF ikatafsiri tukio hilo kama 'tukio la kusababisha ugomvi wakati wa mchezo' na adhabu yake ni kufungiwa mechi mbili hadi tatu.

Uongozi wa klabu hiyo umepanga kukata rufaa ya adhabu aliyopewa nyota wao.

Kwenye mechi hiyo Barcelona walifungwa mabao 3-2 na kulikosa kombe.