Mbappe, Neymar watakavyoshika usajili 2021

Muktasari:

Staa Neymar amewapa matumaini PSG kwa kusema kwamba ana furaha kuwapo Ufaransa, lakini anatakiwa sana arudi Barcelona.

LONDON, ENGLAND

SAFARI moja huanzisha nyingine. Hicho ndicho kitakachokwenda kutokea kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kuhusu usajili wa mastraika bab’kubwa duniani.

Ni hivi. Ishu nzima inaanzia kwa Paris Saint-Germain. Kama mabingwa hao wa Ufaransa, PSG watashinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya basi watabadilisha kabisa mwenendo wa usajili wa mastraika bora kabisa Ulaya.

PSG wameichapa Bayern Munich na kuwatupa nje mabingwa hao watetezi na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

Na wanafurahia mafanikio yao ya kutinga nusu fainali kwa taarifa za Neymar kutangaza kwamba atabaki zake Paris, ikiwa ni mpango wake wa kuisaidia PSG kutawala soka la Ulaya kwa miaka kadhaa ijayo.

Rais wa klabu ya PSG, Nasser Al-Khelaifi alitangaza kwamba Neymar na Kylian Mbappe wote watabaki kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa Ufaransa. Na kama lisemwalo litatimia, basi jambo hilo litavuruga uhamisho wa klabu nyingi za Ulaya kwenye mchakato wao wa kunasa mastraika wapya dirisha lijalo.

Mbappe anasakwa sana na Real Madrid, hivyo kama ataamua kubaki PSG, basi Los Blancos hawatakuwa na namna nyingine zaidi ya kuhamishia nguvu kubwa kwa straika wa Borussia Dortmund, Erling Haaland.

Lakini, Haaland yupo pia kwenye rada za Manchester United na Manchester City. Kuna taarifa ziliwahi kufichua kwamba Haaland mwenyewe anataka kwenda kukipiga Hispania, hasa Santiago Bernabeu.

Mabosi wa Barcelona nao wanamtaka Haaland wakiamini wanaweza kumtumia kama chambo cha kumbakiza supastaa Lionel Messi kwenye kikosi chao. Na kama Mbappe atasaini dili jipya PSG, basi jambo hilo litapandisha sana thamani ya Haaland, huenda akauzwa hadi Pauni 200 milioni kwa timu itakayomtaka mwishoni mwa msimu huu.

Supastaa, Lionel Messi anamtaka Neymar arudi Nou Camp wakakipige pamoja kama zamani. Lakini, kama Mbrazili huyo ataamua kubaki zake Paris na kumshawishi Messi akaungane naye PSG, basi chochote kinaweza kutokea kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, ikizingatiwa Messi atapatikana bure kabisa.

PSG na Man City ndizo timu mbili zinazomsaka Messi na ndiyo zenye uwezo wa kumudu mshahara wake, usiopungua Pauni 600,000 kwa wiki. Na hapo litakuwa suala la Messi kuamua kwenda kuungana na Neymar na Muargentina mwenzake, Mauricio Pochettino huko PSG, au kwenda kuungana na kocha wake za zamani, Pep Guardiola huko Etihad, ambako atapishana na swahiba wake wa miaka mingi, Muargentina mwenzake, Sergio Aguero.

Kama Messi ataamua kwenda PSG, Haaland akiamua kwenda Real Madrid, Man City haitakuwa na chaguo jingine la straika wa kiwango cha dunia kwenye dirisha lijalo zaidi ya kwenda kumsajili Harry Kane, ambaye pia anasakwa na mahasimu wao, Man United. Vita ya Kane itakuwa ya timu tatu, Man City, Man United na Tottenham wenyewe watakaopambana abaki kwenye kikosi chao na asihamie kwa wapinzani ndani ya Ligi Kuu England.

Barcelona pia nao watafuatilia kwa karibu ishu ya Kane, hasa kama watakuwa wamempoteza Messi. Straika mwingine atakayeingizwa kwenye mduara huo ni Romelu Lukaku, ambaye amekuwa akisakwa na Man City na vigogo wa Hispania.

Hii kitu itaanzishwa kama Mbappe na Neymar watabaki PSG. Jambo hilo litavuruga uhamisho wa vigogo wengi barani Ulaya, kitu kitakachowaweka Liverpool kwenye wakati mgumu pia wa kubaki na huduma za washambuliaji wake, Sadio Mane na Mohamed Salah na huenda ikawahusu pia Arsenal wakawa kwenye hatari ya kumpoteza nahodha wao, Pierre-Emerick Aubameyang akanaswa na vigogo vya Hispania. Ni suala la kusubiri na kuona.