Mbappe akija huku mtaomba poo!

Wednesday October 06 2021
mbape pic

PARIS, UFARANSA. SUPASTAA Kylian Mbappe ni kama anawaita Real Madrid “njooni”.

Staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 22 yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake huko Paris Saint-Germain na hana mpango wowote wa kuongeza dili kuendelea kubaki Parc des Princes.

Mbappe alifichua kwamba Julai mwaka huu alipeleka ombi kwa mabosi wa PSG wamruhusu kuondoka, lakini waliweka ngumu hata Los Blancos ilipokuja na mkwanja mrefu dirisha lililopita la usajili wakihitaji saini yake. Mbappe aliiambia RMC Sport: “Niliomba kuondoka, niliweka wazi sitaki kusaini mkataba mpya, nilitaka timu ipate pesa za kusajili wachezaji wengine wazuri.

“Timu ime-nipa mambo mengi sana. Siku zote nimekuwa na furaha hapa, kwa miaka minne yote niliyokuwa hapa na bado nipo. Niliiambia klabu mapema sana, hivyo ilipaswa kuchukua hatua mapema.”

Madrid walihitaji saini ya Mbappe dirisha lililopita, lakini ofa zao zote zilipigwa chini na PSG. Lakini, sasa baada ya maneno ya Mbappe, hilo lina maana kwamba ameshafungua milango ya kutimkia Bernabeu. Chama hilo la Carlo Ancelotti limepoteza mechi mbili zilizopita, kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sheriff kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kisha ikachapwa tena na Espanyol kwenye La Liga. Ujio wa Mbappe utakuwa habari njema Los Blancos, lakini hazitakuwa taarifa nzuri Eden Hazard.

Staa huyo Mbelgiji maisha yake yameshakuwa magumu mbele ya Vinicius Jr, hivyo akija na Mbappe itakuwa mbaya zaidi. Mbappe ataifanya Madrid kuwa moto kabisa kwa kuwa na kikosi cha kibabe ambapo msimu ujao golini atakuwa kipa Thibaut Courtois, atakayelindwa na mabeki Dani Carvajal, Eder Militao, David Alaba na Ferland Mendy, huku Marcelo na Nacho watasubiri benchi. Kwenye kiungo kuna Casemiro, Toni Kroos na Luka Modric, huku Eduardo Camavinga na Fede Valverde wakijiweka tayari kuwabadili.

Advertisement

Vinicius Jr anatarajia kuanza winga ya kushoto, wakati Rodrygo kulia. Karim Benzema yupo vizuri ila Mbappe kumtoa mmoja eneo hilo la fowadi.

Advertisement