Matumaini mapya yaonekana safu ya ulinzi Man U

Muktasari:

WASHAMBULIAJI wanashinda mechi, mabeki wanashinda mataji, “hii ni moja kati ya kauli maarufu iliyowahi kutolewa na kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson.

WASHAMBULIAJI wanashinda mechi, mabeki wanashinda mataji, “hii ni moja kati ya kauli maarufu iliyowahi kutolewa na kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson.

Wakati huo Sir Alex alikuwa na Man United ambayo ukitafuta orodha ya mabeki watano bora duniani ilikuwa lazima utalitaja jina la mmoja kutoka kwenye kikosi chake.

Kizazi hicho kilimalizikia kwa kina Nemanja Vidic na Rio Ferdinand. Hapakuwahi kutokea tena mabeki walioshusha presha za mashabiki pale Man United. Zilipita saa, siku, wiki, miezi na miaka kadhaa kabla ya kutokea kizazi cha sasa ambapo unaowaona kina Raphael Varane, Tyrell Malacia, Diego Dalot na Lisandro Martinez.

Licha ya kuruhusu mabao mengi kwenye mechi za mwanzoni, moja kati ya maeneo yanayoonekana kuwa bora kwenye kikosi cha Manchester United ni lile la ulinzi tofauti na msimu uliopita.

Ngoja nikwambie kitu safu ya ulinzi ya Man United ya misimu kadhaa nyuma haina tofauti kabisa na safu ya ulinzi ya Manchester City. Usishangae.

Kuna kitu kimoja tu. Kitu kinachoifanya safu ya ulinzi ya Man City isionekane kuwa ni chujio ni uwepo wa wachezaji wengi wanaoweza kukaba kuanzia juu kwenye safu ya ushambuliaji sambamba na viungo wakabaji wenye uwezo mkubwa. Manchester United ilikosa wachezaji wa aina hii.

Wakati Pep Guardiola anaingia Man City alitumia zaidi ya Pauni 150 milioni kusajili mabeki wapya ambao walikuwa ni pamoja na John Stones.

Hata hivyo bado kukawa na makosa mengi kwenye eneo hilo na kusababisha minong’ono iwe mingi.

Lakini siku hadi siku mabeki hawa wakaonekana kuendana na kasi. Sio kwamba walibadilika na kuwa bora ni kwa sababu ya aina ya mfumo ambao ulikuwa unatumiwa na kocha huyu.

Kiwango cha mabeki wa sasa wa Man United ni ishara kwamba mabeki hao wamefanikiwa kwenye kitu kimoja. Kwenye kanuni za kuzuia kuna kitu kinaitwa ‘depth’ ikiwa na maana ya wingi wa wachezaji wa timu husika wakati wa kuzuia.

Man United imekuwa inakosa kiungo ambaye anaweza kupunguza kasi ya mashambulizi katika eneo la mbele ya safu yao ya ulinzi, hivyo mipira mingi imekuwa ikifika kwa urahisi kwenye safu yao ya ulinzi.

Kitu ambacho kilikuwa kinasababisha timu hii isiwe na mwenendo mzuri awali ilikuwa ni baada ya mipira kufika kwa wingi kwenye eneo la ushambuliaji, beki aliyekuwa kiongozi wakati huo Harry Maguire alikuwa anafanya uamuzi wa haraka wa kucheza hatari hizo wakati ambao hakuna ‘depth’ yaani watu wa kulinda nafasi aliyotoka.

Hili unaweza ukaliona pia kwenye mechi iliyopita akiwa na timu ya taifa ya England dhidi ya Ujerumani iliyomaliza kwa sare ya mabao 3-3. Kwa sasa waangalie Lisandro Martinez na Varane wamekuwa na aina hiyo ya uchezaji.

Staili ya uchezaji ya Man United haijabadilika, lakini wao wamebadilisha staili ya uchezaji wa safu ya ulinzi timu.

Uzoefu wa Varane nao umekuwa moja ya silaha kubwa kuboresha zaidi safu hiyo ya ulinzi ambayo inaonekana kurudisha matumaini siku hadi siku. Kila la heri kwao!