Maradona dakika chache kabla ya kifo

Muktasari:

  • Aliongoza nchi yake kufika fainali ya Kombe la Dunia 1990 huko Italia, ambapo walifungwa na Ujerumani Magharibi, kabla ya kwenda kuwa nahodha wa miamba hiyo katika fainali za Marekani mwaka 1994, lakini alirudishwa nyumbani baada ya kushindwa kwenye vipimo vya dawa za kuongeza nguvu.

TIGRE, ARGENTINA. MASHABIKI wa soka duniani wapo kwenye majonzi kutokana na kifo cha gwiji wa mchezo huo kutoka Argentina, Diego Maradona kukumbwa na mauti akiwa na umri wa miaka 60.
Maradona anayekumbukwa kwa bao lake la mkono alilowatungua Waingereza kwenye mechi9 ya robo fainali ya Kombe la Dunia 1986 kisha kuwafunga mdomo kwa kuipangua ngome nzima ya Three Lions akiwamo kipa na kufunga bao tamu, alifariki dunia jana baada ya kupata mshtuko wa moyo.
Kifo chake kimejiri ikiwa ni kama wiki mbili tu tangu alipofanyiwa upasuaji wa kuondoa damu iliyoganda kwenye ubongo wake na kisha kuruhusiwa kurudi nyumbani kabla ya jana hali yake kubadilika na kuiaga dunia, kifo kilichoshtua mastaa mbalimbali duniani.
Kabla ya mauti kumkumba, gwiji huyo amekuwa akipambana kuhusu afya yake akiripotiwa kwenda hospitali mara nyingi huku mwezi uliopita akitimiza umri wa miaka 60.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya gwiji huyo aliyetamba na jezi namba 10 na ambaye amekuwa akishindanishwa na mkali mwingine wa duniani kutoka Brazil, Pele mapema jana Jumatano asubuhi, alipata kifungua kinywa akiwa na mpwa wake Johnny Esposito.
Inaelezwa mara baada ya mlo huo, Maradona aliaga kwamba anakwenda kulala, lakini dakika chache baadae hali yake ilibadilika na wana familia na wale wanaomuuguza wakajaribu kumsaidia kuokoa uhai wake na inaelezwa neno lake la mwisho kulitoa lilikuwa 'najisikia vibaya'.
Baada ya hali hiyo kubadilika, inaelezwa aliitwa nesi ambaye alijaribu kumtibia kwa dakika kadhaa, kabla ya kuchukua maamuzi ya kuita gari ya wagonjwa lakini walishachelewa kwa sababu fundi huyo wa mpira alipoteza maisha kabla hata ya gari ya wagonjwa kufika.

Maradona dakika chache kabla ya kifo


Maradona aliyezichezea klabu mbalimbali ikiwamo Barcelona na Napoli, alijizolea umaarufu kutokana na maisha yake kujawa matukio ya kusisimua na kuvutia ikiwamo kutumia dawa za kulevya, kuabudiwa kama mungu na pia kuwa mtu wa kula bata hadi katika uzee wake, huku akijishughulisha na soka karibu sehemu kubwa ya maisha yake.
Tukio kubwa zaidi kwake na ambalo liliwachukiza Waingereza ni lile la kuwatungua kwa bao la mkono, kisha alipohojiwa alidai lile lilikuwa bao la mkono wa Mungu, lakini kila wakirejea kuangalia namna alivyoidhalilisha ngome ya timu yao ya taifa alipowafunga bao la pili, wanajikuta wanatulia kwani enzi zake, Maradona alikuwa ni fundi haswa wa soka uwanjani.