Manchester City ilivyobeba pointi za ubingwa EPL

Muktasari:

MANCHE-STER City wametangazwa mabingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya mahasimu wao waliokuwa wakiwacheleweshea sherehe za kubeba taji, Manchester United kuchapwa na Leicester City uwanjani Old Trafford.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHE-STER City wametangazwa mabingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya mahasimu wao waliokuwa wakiwacheleweshea sherehe za kubeba taji, Manchester United kuchapwa na Leicester City uwanjani Old Trafford.

Chama hilo la kocha Pep Guardiola limenyakua taji la tatu la ligi ndani ya misimu minne, huku msimu huu pengo la kibabe la pointi 10 kileleni likiwapa ubingwa wa msimu huu baada ya Man United kuonekana kuchelewesha sherehe.

Man City iliamini ingebeba ubingwa Jumamosi iliyopita, lakini wakakutana na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Chelsea. Baada ya hapo walisubiri Man United ipoteze mechi yake dhidi ya Aston Villa Jumapili, lakini mambo yalikuwa tofauti, wakashinda 3-1 na kufanya sherehe za Etihad zizidi kuchelewa.

Lakini, usiku wa juzi Jumanne utata ulimalizika rasmi kwa Man City kubeba taji lao baada ya Man United kuchapwa 2-1 na Leicester City, Caglar Soyuncu akifunga kwa kichwa bao la ushindi kwenye kipindi cha pili na hivyo kuwafanya wababe hao wa Etihad kuwavua rasmi ubingwa wa ligi Liverpool.

Hilo ni taji la tisa la ligi kubebwa na Guardiola katika maisha yake ya ukocha, ambapo alibeba mara tatu na Barcelona, mara tatu na Bayern Munich na sasa mara tatu akiwa na Man City.

Hivi ndivyo Man City ilivyonasa pointi 80 zilizotosha kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, huku wakiwa na mechi tatu mkononi.


SEPTEMBA 2020, POINTI 3

Katika mwezi wa kwanza kabisa wa Ligi Kuu England msimu huu, Manchester City ilicheza mechi mbili na kuvuna pointi tatu. Mechi yake ya kwanza ilianza kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Wolves ugenini, kabla ya kuchapwa 5-2 na Leic-ester City nyumbani Etihad. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mabingwa hawa wapya wa ligi msimu huu.


OKTOBA 2020, POINTI 8

Katika mwezi wa pili wa msimu huu wa Ligi Kuu England baada ya kuanza, Manchester City ilicheza mechi nne na kuvuna pointi nane. Ilianza kwa sare ya 1-1 na Leeds United kabla ya kuichapa Arsenal 1-0 uwanjani Etihad. Baada ya hapo ilipata sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United kabla ya kufunga mwezi huo kwa kuichapa Sheffield United 1-0 kwao. Kwa mwezi huo, chama hilo la Pep Guardiola kuvuna pointi nane.


NOVEMBA 2020, POINTI 4

Man City ilianza Novemba kwa sare katika mechi zao za Ligi Kuu England, wakati ilipotoa sare ya 1-1 na waliokuwa mabingwa watetezi Liverpool uwanjani Etihad. Baada ya hapo, miamba hiyo ilikwenda kukumbana na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur, kabla ya kwenda kumalizia hasira zao kwa Burnley wakati ilipowakung’uta 5-0 kwenye mchezo mkali kabisa wa ligi hiyo uliofanyika Etihad. Hadi hapo, Man City ilikuwa bado haijaonyesha dalili kabisa za kwenda kuwa mabingwa wa ligi hiyo ya kibabe kabisa msimu huu.


DESEMBA 2020, POINTI 11

Katika mwezi wa Desemba, Man City ilicheza mechi tano za Ligi Kuu England na kufanikiwa kuvuna pointi 11 kati ya 15. Chama hilo la Guardiola lilianza mwezi huo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham uwanjani Etihad kabla ya kwenda Old Trafford kuwakabili Manchester United na kuambulia pointi moja baada ya kutoka suluhu. ManCity ilipata sare nyingine ya pili mfululizo baada ya kutoka sare ya 1-1 na West Brom, kabla ya kuwachapa 1-0 Southampton na kisha kuwachapa Newcastle United 2-0.


JANUARI 2021, POINTI 18

Man City ilianza mwezi wa Januari mwaka huu kwa kasi kubwa na kushinda mechi zake zote sita ilizocheza kwenye Ligi Kuu England na hivyo kuvuna pointi 18, ambazo zilianzisha mwanzo mzuri kwenye duru ya pili na kwenda kuchukua ubingwa. Man City ilianza kwa kuichapa Chelsea 3-1 Stamford Bridge, kisha ikaichapa Brighton 1-0, Crystal Palace 4-0, Aston Villa 2-0, West Brom 5-0 na Sheffield United 1-0 na hivyo kuwasha moto kwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo.


FEBRUARI 2021, POINTI 18

Pep Guardiola aliendelea kuwasha moto kwenye Ligi Kuu England baada ya kushinda mechi zote za ligi hiyo ambazo timu yake ya Man City ilicheza kwenye mwezi wa Februari mwaka huu. Katika mechi huo, Man City ilicheza mechi sita na kushinda zote. Walianza kwa kuichapa Burnley 2-0 kabla ya kwenda kuibabua Liverpool 4-1 uwanjani Anfield. Baada ya hapo ilicheza dhidi ya Tottenham Hotspur na kushinda 3-0, matokeo ya kulipa kisasi kabla ya kuchapwa wababe wengine wa Merseyside, Everton 3-1 na kwenda kuwababua 1-0 Arsenal kwenye uwanja wao wa Emirates na kumalizia mwezi huo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Ham United.


MACHI 2021, POINTI 9

Mwezi Machi, Man City ilicheza mechi nne kwenye Ligi Kuu England na kuvuna pointi tisa. Jambo hilo lilionyesha ubora wao na dhamira katika kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo baada ya kupoteza pointi tatu tu kwa mwezi huo. Man City iliianza kwa kuichapa Wolves 4-1 ikiwa ni ushindi wa pili kwa timu hiyo kwa msimu huu. Mechi iliyofuatia ilikuwa ni Manchester derby na hapo, Man City ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu Man United kabla ya kuzichapa Southampton 5-1 na Fulham 3-0 ugenini.


APRILI 2021, POINTI 6

Aprili, Man City ilicheza mechi tatu za Ligi Kuu England na kufanikiwa kushinda mbili tu na kukumbana na kichapo kwenye mchezo mmoja. Pep Guardiola hakuwa na ujanja mbele ya Marcelo Bielsa na chama lake la Leeds United, wakati alipokubali kichapo cha mabao 2-1. Mechi nyingine mbili, Man City ilikipiga na Leicester City uwanjani King Power na kushinda 2-0 na pia waliichapa Aston Villa ya Jack Grealish mabao 2-1 uwanjani Villa Park. Kwa pointi ilizokusanya hadi wakati huo, Man City tayari ilikuwa imejiweka kwenye wakati mzuri kabisa wa kunyakua ubingwa.


MEI 2021, POINTI 3

Man City bado ina mechi tatu za kucheza kukamilisha msimu huu wa Ligi Kuu England. Kwa mwezi huu wa Mei, miamba hiyo ya Etihad tayari imecheza mechi mbili na kuvuna pointi tatu. Ilianza mwezi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crystal Palace ugenini, lakini baadaye ilikwenda kukumbana na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Chelsea, tena mechi hiyo ikipigwa Etihad. Hata hivyo, hiyo haikuwa tatizo, kwani pengo la pointi 10 limetosha kuwafanya wababe hao kutangaza ubingwa wa ligi, ikiwa ni taji lao la pili la ligi ndani ya misimu mitatu na la tano katika miaka 10. Mechi za Man City zilizobaki kukamilisha msimu huu watacheza na ugenini dhidi ya Newcastle United na Brighton, kabla ya kurudi Etihad kucheza mechi yao ya mwisho dhidi ya Everton kukamilisha ratiba.