Man UTD, Liverpool ngoma ngumu, Solskjaer autaja Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Liverpool na  Manchester United wametoshana nguvu  kwa kutoka suluhu kwenye uwanja wa  Anfield katika michezo ya Ligi Kuu England kwa mara ya  tatu ndani  ya msimu mitano iliyopita. Rekodi imeandikwa.

LIVERPOOL, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema vijana wake wamepoteza jana, Jumapili  fursa  ya kuifunga Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England ambao ulimalizika suluhu  (0-0).

Liverpool, bila ya  kuwa na beki wa kati alisia iliweza kuizuia Manchester United kupata bao kwenye mchezo huo ambao ulichezwa Anfield. Klopp aliendelea kuwatumia Jordan Henderson na Fabinho  kutokana na kusumbuliwa na majeraha kwa mabeki wake wa kati.

Solskjaer amesema, "Ilikuwa ni fursa lakini tumeipoteza ila  lazima tukumbuke kuwa tulicheza na timu nzuri, sikufurahishwa ila bado tumo na haikuwa mbaya sana kwa sababu tulipata pointi na sio mbaya kama tutashinda mchezo ujao,"

“Kuna kazi kubwa sana imefanyika katika kuwa nafasi tuliyopo kwasasa, lakini ni kama kupanda Mlima Kilimanjaro au Evarest na kufika kileleni na kuamua kukaa kupumzika, nini kitatokea? Unaganda hadi kufa” alisema Ole.

Na kupitia ukurasa wa Twitter wa Tanzania National Park (Tanapa) wamempongeza kocha huyo kwa kuongoza Ligi ya Uingereza na kufananisha hatua hiyo kama kuipanda Mlima Kilimanjaro uliopo Tanzania, pia wameshukuru na kumkaribisha nchini Tanzania kufanya utalii.

Upande wake kocha wa Liverpool,Jurgen  Klopp amesema, "Kiwango hakikuwa kibaya kiasi cha kushinda mchezo,  kilikuwa kizuri lakini ili ushinde mchezo unatakiwa kufunga hicho ndicho kitu kilichokosekana ndio maana tulishindwa kuibuka na ushindi."

Manchester United bado wapo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England kwa utofauti wa pointi mbili dhidi ya Manchester City, ambao wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 35 baada ya kuifunga Crystal Palace mabao  4-0.

Leicester City ambao kesho, Jumanne wataikaribisha Chelsea kwenye mchezo wao ujao wa Ligi wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na pointi 35, Liverpool wao wameshuka hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi 34.