Man United msikieni Bruno Fernandes
Muktasari:
- Mastaa wa Man United walifanya makosa ya kizembe sana kwenye mechi hiyo na kujikuta wakichapwa 3-0 na wapinzani wao hao wakubwa kwenye Ligi Kuu England.
LISBON, URENO: NDO hivyo. Bruno Fernandes amekiri kwamba Manchester United haipo tayari kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kipigo ilichopata kutoka kwa Liverpool.
Mastaa wa Man United walifanya makosa ya kizembe sana kwenye mechi hiyo na kujikuta wakichapwa 3-0 na wapinzani wao hao wakubwa kwenye Ligi Kuu England.
Man United haikuonekana kuwa tishio lolote kwenye fowadi yao katika mechi hiyo jambo linalomfanya Fernandes kukiri kwamba bado wapo nyuma sana kwenye ishu ya kuwa washindani kwenye mbio za ubingwa.
Alisema mpango wa sasa wa timu hiyo ni kumaliza ndani ya Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, akisisitiza timu yake bado haina uwezo wa kuwania taji.
Fernandes aliambia DAZN huko Ureno: “Ndiyo, nafahamu wazi Manchester United hii haipo tayari kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England.
“Sawa, tunapambania ubingwa lakini kwa ukweli wa kujaribu kuwamo kwenye nne bora, nafasi ambayo itatupa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, kuna mengi ya kuyaboresha, ndoto zangu ni kushinda ubingwa siku moja.”€
Fernandes, 29, hakuwa kwenye ubora wake katika mechi hiyo ya Liverpool na kocha wa zamani wa Ligi Kuu England, Alan Pardew anaamini mchezaji huyo anapaswa kuvuliwa kitambaa cha unahodha.
Pardew alisema: “Sikumwona kabisa Fernandes kwa sababu hakuwa na mpira. Kwenye kulinda, hayupo vizuri kabisa. Anawezaje kuongoza timu?.”