Man United ikiteleza tu, Inashushwa na Man City

MANCHESTER, ENGLAND. MAMBO yanaenda kuwa magumu kwa Manchester United ambao mwishoni mwa wiki walitoka kupata sare ya 0-0 dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.

Ugumu unakuja kutokana na wapinzani wao kutoka jiji moja la Manchester, Manchester City ambao leo inashuka dimbani kumenyana na Aston Villa mchezo unaotarajiwa kupigwa katika dimba la Etihad saa 3:00 usiku na ikifanikiwa kushinda itapanda hadi kileleni.

Man City inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 35 baada ya kucheza mechi 17, ikishinda 10, sare tano na kufungwa mbili.

Wakati huo Man United inashika nafasi ya kwanza kwa alama 37, ilizokusanya baada ya kucheza mechi 19, ikishinda 11, sare nne na kufungwa tatu.

Hivyo, Man City ikishinda itakaa kileleni kwa tofauti ya alama moja wakati huo itakuwa na faida ya mchezo mmoja mkononi.

Man City imekuwa katika kiwango bora kwenye siku za hivi karibuni na imefanikiwa kushinda mechi tano mfululizo zilizopita.

Lakini hiyo haiondoi ubora wa mpinzani wake Aston Villa iliyo na makali zaidi ikikutana na timu zinazoshika nafasi sita za juu kwa msimu huu kwani ilimfunga Liverpool mabao 7-2.

Lakini kwenye mechi chache zilizopita haijafanyi vizuri kwa sababu wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wamekumbwa na maambukizi ya virusi vya Corona, hali iliyosababisha iwe kwenye nafasi ya 11 baada ya kucheza mechi 15 ikishinda nane, sare mbili na kufungwa tano na katika mechi tano za mwisho imefungwa moja, sare mbili na kushinda mbili.

Katika mchezo huo, Kocha wa Man City, Pep Guardiola alisema: “Sijihitaji kutuma meseji yoyote kwa Villa, wiki chache zilizopita tulikuwa nyuma ya Liverpool lakini tumeshinda mechi chache zilizopita zilizotufanya kuwa kwenye nafasi tuliyopo kwa muda huu, pia bado nafikiria kuhusu Villa wakati huu ninaoendelea kunywa kinywaji kukamilisha sherehe zangu za siku ya kuzaliwa,” alisema Guardiola ambaye Jumatatu iliyopita alitimiza umri wa miaka 50.

“Tutajaribu kucheza tofauti na msimu uliopita ili kuhakikisha hatufanyi makosa mengi kwenye eneo la mwisho,” aliongeza.

Vile vile, akaongeza kuhusu kiwango cha John Stone akisema kama kuna wachezaji anafurahi kuwaona uwanjani kwa sasa ni beki huyo kwani anafanya kile anachomtuma kwa asilimia nyingi.

Mara ya kwanza timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 1899 na Man City imeshinda mara 75, huku 41 zikimalizika kwa sare na Villa ikashinda mara 57.

Katika mechi tisa za mwisho Villa haijawahi kupata ushindi mbele ya wababe hao wa Jiji la Manchester

Rekodi zinaonyesha Villa mara ya mwisho kuifunga Man City ilikuwa ni Septemba 2013 katika dimba la Villa ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-2, baada ya hapo imekuwa ikipata vipigo mfululizo na iliambulia sare kwenye mchezo mmoja uliopigwa Novemba, 2015.

Kwa upande wake kocha wa Villa Dean Smith anasema wachezaji waliokuwa karantini baada ya kukutwa na maambukizi ya Corona wamepona na walishaanza mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa leo.

Man United wenyewe watakuwa ugenini dhidi ya Ful;ham mchezo utakapigwa saa 5:15 usiku na itatakiwa kupata ushindi huku ikiombea Man City ipoteze au itoke sare ili kuiondolea presha ya kushuka nafasi moja chini.

Itakuwa ikitafuta ushindi baada ya mchezo uliopita kuilazimisha liverpool sare ya bila kufungana kwenye Uwanja wa Anfield na kuendeleza rekodi ya kutopoteza ugenini.