Man City, Aguero wamalizana. Messi, Lukaku watajwa

MANCHESTER, ENGLAND. MWISHO wa enzi. Dirisha lijalo la majira ya kiangazi kuna ndoa nyingi za wachezaji na timu zitakwenda kuvunjika. Ndoa hizi zilidumu kwa muda mrefu sana na zilizaa matunda.

Taarifa kutoka jijini Manchester pale England zinadai mabosi wa Manchester City wamempa Pep Guardiola Pauni 200 milioni kama fungu la usajili katika dirisha hilo.

Wakati huo, ndoa ya mfungaji bora wa muda wote wa timu hiyo fundi kutoka Argentina ikitajwa kuwa kwenye hatihati ya kuvunjika.

Aguero mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na hadi sasa hajasaini mkataba mpya kutokana na masharti magumu aliyowekewa.

Man City imemwambia akihitaji wampe mkataba mpya basi akubali kukatwa asilimia 50 ya mshahara wake wa sasa wa Pauni 260,000 kwa wiki.

Lakini hiyo huenda isiwe shida kwake kwani Barcelona na PSG zimeonekana kuwa kwenye harakati za kuiwania saini yake mwisho wa msimu akiwa mchezaji huru.

Tayari Guardiola ameanza kutafuta straika mbadala baada ya kuona uwezekano wa mchezaji huyo kusalia upo kizani na mastaa walio kwenye rada zake ni Lionel Messi kutoka Barca, Romelu Lukaku wa Inter Milan, Erling Haaland wa Dortmund na Darwin Nunez wa Benfica.

Lukaku alicheza EPL kabla ya kwenda Serie A, akiwa amepita Everton, Manchester United na Chelsea na alihudumu Jjjini Manchester kati ya mwaka 2017 hadi 2019.

Hata hivyo, hakuwa na kiwango kizuri tangu alipojiunga na United katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2017 kwa Pauni 90 milioni akitokea Everton, alifunga mabao 42 katika mechi 96 za michuano yote.

Baada ya hapo alijiunga na Inter katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2019 kwa Pauni 72 milioni hadi sasa amecheza mechi 73 za michuano yote na kufunga mabao 51.

Vile vile Kuondoka kwa Aguero kunatoa ishara ya dili la Lionel Messi kuwa kwenye hatua nzuri ndio maana wamempunguzia mshahara ili kupunguza matumizi kwani Messi mshahara wake ni mkubwa sana.

Mchezaji mwingine aliye kwenye hati hati ya kuondoka katika viunga hivyo ni kiungo mkabaji Fernandinho aliyecheza mechi 300 tangu ajiunge nao mwaka 2013.

Maeneo mengine ambayo Guardola anataka kusajili wachezaji wapya ni beki wa kushoto baada ya Benjamin Mendy kuandamwa sana na majeraha.

Vile vile mabeki wa kati Oleksandr Zinchenko na Nathan Ake hawaonekani kuwa kwenye mipango yake ya muda mrefu ukizingatia Eric Garcia huenda akaondoka baada ya kugoma kuongeza mkataba mpya.

Novemba mwaka jana Guardiola alirefusha mkataba wake wa kuendelea kuitumikia City kwa miaka miwili zaidi.

Hiyo ni baada ya mabosi kuridhishwa na kiwango chake akichukuwa mataji mawili ya Ligi Kuu England, matatu ya Carabao Cup na moja la FA Cup alilochukuwa mwaka 2019.

Tangu asajiliwe kwenye kikosi hicho akitokea Atletico Madrid kwa Euro 40 milioni, Aguero ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu, matano ya EFL na moja la FA Cup na ndio anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kufunga mabao 221.

Lakini amefikia hali hiyo kutokana na majeraha ya mara kwa mara anayopata yanayosababisha akae nje kwa muda mrefu.