Lamine Yamal: Mwafrika anayeibeba Uhispania Euro 2024

Winga wa Uhispania, Lamine Yamal akiwa amebeba tuzo ya mchezaji bora wa mchezo baina ya Ufaransa wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutinga fainali ya Euro 2024.

Muktasari:

  • Lamine Yamal ameandika rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga bao katika mashindano ya Euro hatua ya nusu fainali akiwa na miaka 16.

Dortmund, Ujerumani. Dunia nzima hivi sasa inataja jina la kinda wa Uhispania, Lamine Yamal ambaye jana usiku aliiongoza timu ya taifa ya nchi yake kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya (Euro 2024) baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ufaransa.

Katika umri wa miaka 16 na siku 362, Yamal aliirudisha mchezoni Uhispania iliyokuwa imetanguliwa kwa bao moja, baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 21 kabla ya dakika nne baadaye, Dani Olmo kupachika la pili lililoihakikishia Hispania kuingia hatua ya fainali.

Akiwa pembezoni mwa uwanja baada ya kupokea pasi kutoka kwa Alvaro Morata, Yamal alijitengea mpira na kuupiga kwa mguu wake wa kushoto akitumia staili ya kuzungusha kuulekeza langoni mwa Ufaransa ambapo ulimshinda kipa Mike Mignan na kujaa wavuni.

Bao hilo halikuwa na faida kwa Hispania pekee bali pia lilimfanya Yamal kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika mashindano ya Euro.

Ikumbukwe pia tayari mchezaji huyo ameshaichezea Uhispania idadi ya michezo 51 na kuifungia mabao saba.

Hata hivyo wakati Uhispania wakitamba na Yamal ambaye anaichezea pia Barcelona hadithi inaweza kuwa tofauti kwa mataifa ya Guinea ya Ikweta na Morocco ambayo pengine leo hii mojawapo lingekuwa linafaidi huduma ya kinda huyo uwanjani kama ilivyo kwa Hispania ambayo anaichezea hivi sasa.

Yamal angeweza kuichezea Guinea ya Ikweta kwa vile mama yake ni raia wa nchi hiyo pia kama ilivyo kwa Morocco ambayo baba yake anatokea.

Winga huyo ambaye ni mzaliwa wa kitongoji cha Rocafonda 304 ambacho kipo ndani ya jiji la Barcelona akiwa na umri wa miaka saba akiwa anacheza soka mtaani kwenye sakafu alionekana na skauti wa timu ya Barcelona ambaye alivutiwa na kipaji chake na baada ya kupeleka taarifa zake, klabu hiyo iliwasiliana na baba yake ili kumshawishi amruhusu kujiunga na kituo chao cha soka kwa vijana wadogo cha La Masia.

Baba yake ambaye aliongozana naye hadi katika makao makuu ya klabu hiyo, aliwapa sharti kuwa kama wanamhitaji mtoto wake achezee timu yao basi wanatakiwa kumsomesha jambo ambalo klabu hiyo iliridhia.

Baada ya hapo kilichobakia ni historia kwani mchezaji huyo amegeuka kuwa lulu katika kikosi cha Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania kutokana na kiwango bora anachoonyesha kwa kufunga mabao au kupiga pasi za mwisho.

Lamine Yamal akichonga mpira uliozaa bao la kusawazisha katikati ya wachezaji wa Ufaransa jana Julai 9, 2024 na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Picha na Mtandao

Rekodi juu ya rekodi

Mbali na rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika fainali za Euro, Yamal pia amekuwa ni mchezaji mdogo zaidi kuichezea Barcelona akiwa na umri wa miaka 15 na siku 290 tangu Armando Sagi alipofanya hivyo mwaka 1922.

Ni mchezaji mdogo zaidi kuanza katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania na pia anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kupiga pasi ya mwisho kwenye ligi hiyo.

Anashikilia pia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika La Liga na pia nyota mdogo zaidi kupiga pasi ya mwisho kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wachezaji wa Uhispania wakishangilia bao lililofungwa na Lamine Yamal katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Ufaransa na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Atabiriwa makubwa

Mshambuliaji wa zamani wa England na Newcastle United, Alan Shearer alisema kuwa Yamal ana kipaji cha kipekee.

"Tumekuwa tukimzungumza kuhusu yeye kwenye mashindano yote na kusema ni mchezaji wa kushangaza katika umri wake," alisema Shearer.

Kocha wa Hispania, Luis de la Fuente alisema kuwa Yamal ni mchezaji ambaye kila wakati anaonyesha ishara za kuwa staa mkubwa siku za usoni.

"Anaonekana ana uzoefu wa kutosha kusema ukweli. Nashangilia kwamba yupo kwenye timu yetu na ni Muhispania," alisema Fuente.