Lahm afunguka mazito kwa Mane

Muktasari:

BEKI wa zamani wa Bayern Munich, Philipp Lahm ametilia shaka nafasi ya Sadio Mane katika miamba hiyo ya Bundesliga.

BEKI wa zamani wa Bayern Munich, Philipp Lahm ametilia shaka nafasi ya Sadio Mane katika miamba hiyo ya Bundesliga.

Nini kimetokea? Mane ambaye aliondoka Liverpool msimu wa majira ya joto baada ya kufunga mabao 120 katika mechi 269 alianza vyema kwenye kikosi cha Bayern Munich alipofunga katika mechi nne mfululizo mwanzoni mwa msimu.

Hata hivyo, bado hajapata bao lingine kwa The Bavarians katika mechi sita zilizopita. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Southampton amefunga mabao matano katika mechi 11 za mashindano yote, lakini ni matatu pekee amefunga kwenye Bundesliga.

Mane amekuwa akitumika zaidi kama mshambuliaji wa kati na wakati mwingine winga wa kushoto, na Lahm anahoji mabadiliko haya ya nafasi kwa Mane.

Kilichosemwa “Sifa za Mane hazina shaka,” Lahm alisema, kama alivyonukuliwa na Liverpool Echo.

“Lakini ni muhimu kwamba majukumu yake lazima yawe wazi. Sioni hilo kwa sasa. Kwa sasa sielewi jinsi majukumu yanavyofafanuliwa. Kila mtu anapaswa kujua anachopaswa kufanya uwanjani.”