Kwaheri! Miaka 19 ya Wayne Rooney uwanjani

MANCHESTER, ENGLAND. HATIMAYE kile kizazi cha dhahabu cha Manchester United kilichoushangaza ulimwengu Old Trafford kinazidi kupotea. Kizazi hicho ni kile cha Rio Ferdinand, Gary Neville, Nemanja Vidic, Patrice Evra ambao wote wamestaafu na sasa Wayne Rooney amefuata nyayo zao.

Rooney ametangaza kustaafu Ijumaa iliyopita akiwa na Derby County ambayo imempa mkataba wa kuwa kocha mkuu baada ya kuhudumu kama kocha wa muda kwa miezi kadhaa tangu afukuzwe Philip Cocu.

Anastaafu huku akiacha rekodi ya kukumbukwa daima kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya England akiingia kambani mara 53, sambamba na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Man United akiingia kambani mara 253.

Jina lake liliandikwa kuanzia Oktoba, 2002 pale alipompa tabu David Seaman aliyekuwa kipa wa Arsenal wakati huo.

Rooney alifunga bao la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa kwenye dimba la Goodson Park na akaweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga bao kwenye ligi hiyo, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16 na siku 360.

Goli hilo lilibadilisha taswira ya maisha yake ya soka kwani Feburuari 2003 aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England na akacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Australia wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17 na siku 111.

Katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi 2004, Sir Alex Ferguson alijitosa kwenye akamsajili Rooney kwa dau kubwa bila ya kujali ikiwa ataonyesha kiwango kizuri au lah.

Manchester United ilitoa Pauni 30 milioni ili kumnunua na kwenye mechi yake ya kwanza tu alifunga hat-trick katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Fenerbahce ambapo Man United ilishinda mabao 6-2 na akawa mchezaji wa kwanza mdogo kufunga mabao matatu kwenye mechi ya kwanza katika historia ya michuano hiyo.

Rooney alidumu kwa Mashetani Wekundu hadi 2017 akicheza jumla ya mechi 559 na kufunga mabao 253, kisha alirudi tena Everton alipocheza kwa msimu mmoja mechi 40 akiingia kambani mara 11 na baadaye akatimkia Marekani kuitumikia DC United akicheza mechi 52 na kufunga mabao 25.

Mwaka 2020 alitua Derby County imayocheza Daraja la Kwanza England na akahudumu kama kocha mchezaji akicheza mechi 35 na kufunga mabao saba.

Kwa ujumla kwenye kipindi cha miaka 19 aliyocheza klabu hizo nne amecheza mechi 763 na kufunga mabao 313.

Kwa upande wa timu ya taifa ya England alicheza kuanzia 2003 hadi 2018 jumla ya mechi 120 na kufunga mabao 53.

Sir Alex Ferguson aliyewahi kumfundisha huko Manchester United alisema Rooney ni mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kuwashuhudia katika soka.

Vilevile kustaafu kwake na kugeukia masuala ya ukocha ana imani atafanikiwa kwani ana uelewa mkubwa wa masuala ya soka.

“Amepiga hatua kubwa sana na umeona alipopewa timu aifundishe kwa muda alianza vizuri, najua haendi kujaribu anakwenda kufanya, ukiangalia sehemu alizopita zimempika vyema ili kuwa bora,” alisema Ferguson.

Vilevile kocha wa West Ham aliyewahi kumfundisha Everton, David Moyes alisema: ”Inanifanya nifikirie sana maana ni juzi tu nilimpandisha kwenye timu ya wakubwa alipokuwa na umri wa miaka 16 na sasa nasikia kwamba amekuwa kocha mkuu.”

“Ni kweli ana uzoefu mkubwa kama mchezaji, lakini anatakiwa aangalie asije akaangukia kwenye shimo la kuwa mchezaji mzuri asiyekuwa kocha bora, anatakiwa ajifunze mbinu mbalimbali na lazima atambue, hatakiwi kufanya mambo kwa kukurupuka.”

Naye mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya England ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa kituo cha BT Sports, Gary Lineker alisema amestaafu mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote nchini England aliyefanya vitu ambavyo wachezaji wengi wanahitaji kufanya uwanjani.

Rooney aliyestaafu soka akiwa na umri wa miaka 35, alisema licha ya kustaafu kucheza lakini bado anaendelea kusalia kwenye mpira kwa sababu ni moja ya vitu anavyovipenda kwenye maisha yake. “Kitu kikubwa ninachokiangalia ni kuirudisha timu (Derby County) kwenye nafasi za juu na litakuwa ni jambo zuri zaidi,” alisema.