Kvaratskhelia atua kwenye rada za timu vigogo Ulaya
Muktasari:
- Mchezaji huyo ambaye ni tegemeo kwa sasa katika kikosi cha Napoli, huduma yake pia inahitajika na Liverpool.
MANCHESTER United imepanga kuingia kwenye vita dhidi ya PSG ili kuipata huduma ya winga wa Napoli na Georgia, Khvicha Kvaratskhelia, 23, katika dirisha hili la usajili.
Mchezaji huyo ambaye ni tegemeo kwa sasa katika kikosi cha Napoli, huduma yake pia inahitajika na Liverpool.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027 na msimu huu amecheza mechi 19 za michuano yote, akifunga mabao matano na kutoa asisti tatu.
Kwa mujibu wa taarifa Liverpool ipo tayari kumpa ofa ya mshahara mara nne zaidi ya ule ambao anaupokea sasa ikiwa ni harakati za kumshawishi. Awali timu nyingi zilihitaji kumsajili dirisha la majira ya kiangazi lakini ilishindikana baada ya Napoli kugoma kumuuza. Kwa sasa anadaiwa kaomba kuondoka.
Milos Kerkez
WACHEZAJI wanne wa Bournemouth wapo katika rada za timu kubwa za England zinazopambana ili kuwasajili katika dirisha hili au lijalo. Mastaa hao ni pamoja na Illia Zabarnyi, Milos Kerkez, Antoine Semenyo na Dean Huijsen. Timu zinazohusishwa na wachezaji hao ni Chelsea, Newcastle United na Liverpool. Nyota hao wote ni tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Bournemouth.
Marcus Rashford
WEST Ham United imezungumza na wakala wa mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford na kumwambia kuwa ipo tayari kumchukua kwa mkopo wa nusu msimu ikiwa itashindikana kutimkia kwenye timu nyingine kubwa anazohusishwa nazo. Kwa mujibu wa taarifa, West Ham haitaki kuweka nguvu kubwa ingawa itakuwa tayari kumsajili hata dakika za mwisho za dirisha hili.
Bryan Mbeumo
MANCHESTER United imejikuta vitani dhidi ya Arsenal katika harakati za kumsajili mshambuliaji wa Brentford na Cameroon, Bryan Mbeumo, 25, katika dirisha hili. Mbeumo amecheza mechi 23 msimu huu michuano yote na kufunga mabao 13, mkataba wake unamalizika 2026. Arsenal ndio inaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kumsajili.
Vitor Reis
MANCHESTER City inapambana kuhakikisha inakamilisha mchakato wa kumsajili beki wa Palmeiras na Brazil, Vitor Reis katika dirisha hili. Reis mwenye umri wa miaka 18, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kunalizika 2028. Man City iliripotiwa kuanza kumfuatilia tangu mwaka jana wakati hajatimiza umri wa miaka 18.
Harvey Elliott
KIUNGO wa Liverpool na England, Harvey Elliott, 21, yupo kwenye rada za Brighton na Borussia Dortmund zinazohitaji huduma yake katika dirisha hili lausajili ambalo linaendelea huko Ulaya. Elliot amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Liverpool tangu kuanza kwa msimu huu wa mashindano, jambo linalosababisha aombe kuondoka katika dirisha hili.
Aaron Ramsdale
KIPA wa Southampton na England, Aaron Ramsdale, 26, yupo kwenye rada za Newcastle United inayoweza kukamilisha usajili wake katika dirisha hili la usajili huko Ulaya. Ramsdale ambaye ndiye kipa namba moja wa Southampton kiwango chake kimemvutia sana kocha Eddie Howe ambaye amependekeza asajiliwe katika dirisha hili.
Douglas Luiz
NOTTINGHAM Forest inafanya jitihada za kumsajili kiungo wa Juventus na Brazil, Douglas Luiz, 26, kwa mkopo katika dirisha hili, lakini inakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Manchester United, Manchester City na Fulham ambazo zinahitaji huduma ya nyota huyo. Mkataba wa sasa wa Luiz unatarajiwa kumalizika 2027.