Kumbe Lukaku hakuwahi kufunga Stamford Bridge

Monday September 13 2021
lukaku pic

LONDON, ENGLAND. MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Romelu Lukaku baada  ya kutupia mabao mawili dhidi ya Aston Villa kwenye mchezo wa Ligi Kuu England,  amesema kufunga bao kwenye uwanja wa  Stamford Bridge ni kitu ambacho alikuwa akikiota tangu akiwa mdogo.

Mbelgiji huyo alitupia bao lake la kwanza kwenye uwanja huo wa nyumbani wa Chelsea mwanzoni mwa kipindi cha kwanza baada ya pasi nzuri aliyopigiwa na  Mateo Kovacic na kuwafanya matajiri hao wa London kuendelea kutesa kwenye ligi hiyo bila ya kupoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa msimu.

"Ilikuwa ndoto yangu tangu nikiwa na miaka 11. Nilipambana kwa kujitoa kwa ajili ya kipindi hiki, " amesema mshambuliaji huyo mwenye mabao matatu kwenye michezo mitatu aliyoichezea Chelsea tangu arejee akitokea Inter Milan.

Aliongea kwa kusema; "Nilikuwa  na panda shuka  (mwanzoni mwa safari yake)  lakini nimepata uthabiti fulani katika miaka mitatu iliyopita. Kwa uzoefu na bidii, ninaendelea na mapambano.

"Ni mwanzo mzuri lakini lazima tuendelee kupambana. Tunajua mwaka huu utakuwa na ushindani mkubwa. Timu nyingi zitapigania taji."

Lukaku alionekana akibusu nembo ya jezi ya klabu hiyo mara baada ya kufunga bao ambalo liliipa uongozi Chelsea, kiujumla mchezo huo ulikuwa wa 15 kwa mshambuliaji huyo kucheza kwenye uwanja wa  Stamford Bridge.

Advertisement

Mbelgiji huyo alionyesha ubora wa namna yake kwenye kufunga bao hilo kwani baada ya kupigiwa pasi ndefu na Kovacic aliukokota mpira na kuubadili uelekeo kwa kumpiga chenga beki wa Aston Villa, Axel Tuanzebe na kumalizia kirahisi.

Bao la pili alifunga kipindi cha pili akiwa ndani ya penalti box baada ya kupasiwa na nahodha wake, César Azpilicueta alipasia nyavu za juu kushoto mwa kipa wa Aston Villa, Jed Steer na kuifanya Chelsea kupata bao la tatu. Bao la pili lilifungwa na Kovacic

Advertisement